1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasheria wataka ICC ichunguze uhalifu wa kivita Yemen

31 Agosti 2021

Wanasheria wanaowawakilisha wahanga wa vita vinavyoendelea Yemen wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuchunguza matukio ya uhalifu wa kivita yanayofanywa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali.

https://p.dw.com/p/3ziha
Jemen | Gräber von jeminitischen Kämpfern in Marib
Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Jumuiya ya mawakili iitwayo kwa kifupisho cha Guernica 37 ilisema siku ya Jumatatu (Agosti 30) kwamba iliwasilisha ushahidi mbele ya ICC kuunga mkono hoja yao kwamba kumekuwa na matukio ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu yanayotendwa nchini Yemen.

Mawakili hao wenye makao yao jijini London, Uingereza, na ambao wanawawakilisha mamia ya manusura na ndugu wa waliouawa nchini Yemen, wanataka uchunguzi ufanyike hasa juu ya matukio matatu, kwa mujibu wa taarifa waliyoisambaza kwa waandishi wa habari.

Matukio hayo yanajumuisha mashambulizi ya anga yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka 2016, ambayo yaliwauwa watu 140 waliokuwa wakishiriki maziko mjini Sanaa, na mashambulizi mengine kama hayo ya anga dhidi ya basi la skuli kaskazini mwa Yemen, yaliyouwa watoto 40 mnamo mwaka 2018.

Licha ya muungano huo wa kijeshi unaopambana na kundi la Kihouthi kukiri kwamba makosa yalifanyika kwenye mashambulizi hayo na kwamba ungeliwafungulia mashitaka waliohusika, lakini mwanzilishi mwenza wa Guernica 37, Almudena Bernabeu, alisema muungano huo "haukufanya kitu kama hicho."

Mashitaka haya yatafika wapi?

Jemen | al-Suwayda Flüchtlingslager
Mahema kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al-Suwayda nchini Yemen.Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Yemen na Saudi Arabia hazijawahi kusaini Mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, na miongoni mwa mataifa yanayounga muungano huo wa kijeshi, ni Jordan pekee iliyoidhinisha mkataba huo.

Kisheria, ICC haina wajibu wa kuzingatia malalamiko yanayowasilishwa kwa mwendesha mashitaka na watu binafsi ama makundi. 

Mwendesha mashitaka ndiye mwenye mamlak ya kuamua ni kesi ipi ya kuiwasilisha mahakamani, na majaji huamua ikiwa waruhusu uchunguzi wa awali unaofanywa na ofisi ya muendesha mashitaka, na ambao hufuatiwa na uchunguzi rasmi na ikikubalika, mashitaka rasmi kufunguliwa. 

Kwa mujibu wa ICC, kesi nyingi za namna hii huwa hazifikii hatua ya uchunguzi.

Serikali inayotambuliwa kimataifa ya Yemen imekuwa kwenye mapigano na wapiganaji wa Kihouthi tangu mwaka 2014. Saudi Arabia ilishajiisha na hatimaye kufanikiwa kuunda kikosi cha pamoja cha wanajeshi wa mataifa kadhaa ya Kiarabu kuingilia mzozo huo mwaka mmoja baadaye, muda mfupi baada ya Wahouthi kuutwaa mji mkuu wa Yemen, Sanaa.

Tangu hapo, Wahouthi wamefanikiwa kutwaa sehemu kubwa ya upande wa kaskazini, huku maelfu ya raia wakiuawa na mamilioni wakigeuka wakimbizi. Umoja wa Mataifa umeielezea hali ya Yemen kuwa mzozo mkubwa kabisa wa kibinaadamu duniani, huku wataalamu wa Umoja huo wakizituhumu pande zote mbili kwa uhalifu wa kivita.