1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasayansi wa Kiafrika walioko Ujerumani

Bianca von der Au / Maja Dreyer17 Julai 2007

Wakati wanasiasa wanaendelea kujadiliana juu ya sheria ya uhamiaji hapa nchini Ujerumani, kuna malalamiko kutoka vyuo vikuu vya humu nchini kuwa vinakosa wanasayansi kutoka nje. Kwa hivyo vyuo vimeanza kampeni za kuwavutia wanasayansi kuja hapa. Kwa nini basi wasije Waafrika? Kwa sasa kuna wanasayansi 700 wa asili ya Kiafrika wanaofanya utafiti wao Ujerumani. Mwandishi wetu Bianca von der Au amezungumza na baadhi yao ili kufahamu hali yao ilivyo na kuona kuwa maoni yao ni tofauti.

https://p.dw.com/p/CHkA
Idadi ya wanasayansi wa Kiafrika walioko Ujerumani ni ndogo
Idadi ya wanasayansi wa Kiafrika walioko Ujerumani ni ndogo

Wanasayansi wa Kiafrika walioko Ujerumani huwa wanakabiliwa na madhara mengi katika kupanda ngazi katika taaluma. Haya ni maoni ya Bi Maureen Eggers ambaye ni mtaalamu wa mambo ya elimu . Wakati fulani katika kupanda ngazi wanazuiliwa na ukuta wa vioo anasema: “Kwanza kabisa ningesema kuwa bila shaka kuna ubaguzi na kuwa ubaguzi huu unawahusisha makundi fulani. Mimi kama mwanasayansi mweusi wa asili ya Kiafrika ninabaguliwa pia.”

Jina lake kamili ni Maureen Maisha Eggers naye anatoka Kenya. Bi Eggers amefanikiwa kupata nafasi katika chuo kikuu cha Berlin chini ya mradi maalum wa kuwasaidia wanawake. Bila ya mradi huu hangepatiwa nafasi hiyo, anaamini. Mfumo wa vyuo vikuu vya Ujerumani unatawaliwa na mtazamo wa mume mzungu. Kwa hivyo inabidi kuwa na miradi mingine ya kuwasaidia wanasayansi kutoka Afrika, anadai Maureen Eggers: “Matatizo yanatokea hasa baada ya kupata shahada ya udaktari, pale ambapo itabidi kupata nafasi ya kuendelea na utafiti. Hapo nadhani kunatofautishwa kati ya wanasayansi wa asili mbali mbali.”

Mwenye maoni mengine ni Profesa Christophe Bobda wa jumuiya ya wahandisi wa Cameroon nchini Ujerumani. Yeye hajawahi kuzuiliwa katika kupanda ngazi ya kazi. Profesa huyu wa elimu ya uhandisi ana hakika kuwa kinachozingatiwa ni juhudi za kila mmoja pamoja na mafanikio katika utafiti na siyo asili.

Profesa Christophe Bobda amekuja Ujerumani mwaka 1993 na amejifunza lugha ya Kijerumani hapa Ujerumani. Baada ya kusoma masomo ya kompyuta na kupata shahada yake na diploma amepata nafasi ya kuandaa shahada ya udaktari ikifuatiwa na nafasi ya kuwa profesa kijana. Halafu ameitwa katika chuo kikuu cha Potsdam kuchukua cheo cha profesa. Anaeleza: “Mimi binafsi nimeweza kuendelea vizuri. Hapa Ujerumani sijawahi kujisikia kama ninabaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yangu. Watu wote, ikiwa ni wenzangu wa kazi au walio juu nami walitathmini tu kazi niliyofanya.”

Profesa Bobda anasema kuwa ni juu ya wanasayansi wa Kiafrika wenyewe kujitafutia nafasi kwenye vyuo vikuu vya Ujerumani. Sababu kuu ya kushindwa, kama anavyoona Profesa huyu ni lugha ya Kijerumani: “Ni kitu muhimu sana hapa Ujerumani na wengi ambao wanasoma hapa hawatambui kuwa wanahitaji lugha baada ya kumaliza masomo. Ikiwa unataka kuendelea na utafiti lazima uwe na uwezo wa kuzungumzia shughuli yako mbele ya wanafunzi na vile vile kati ya wanasayansi wengine, la sivyo hutafanikiwa.”

Huenda lakini tatizo hili litaondoshwa katika siku za usoni, kwani tayari kwenye vyuo kadhaa humu nchini lugha ya Kiingereza kinatumika katika mafunzo.