1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Rwanda wadai kulazimishwa chanjo ya COVID-19

19 Januari 2022

Ingawa Rwanda ilisema kuwa haitolazimisha watu kupiga chanjo ya corona, lakini baadhi ya wakaazi hususani katika maeneo ya vijijini wamedai kuwa maafisa wa serikali wamekuwa wakiwalazimisha kuchanjwa.

https://p.dw.com/p/45kI0
Afrika Ruanda Kigali Corona Impfung
Picha: Cyril Ndegeya/ Xinhua News Agency/picture alliance

Rwanda imetambuliwa na shirika la afya ulimwenguni kuwa miongoni mwa nchi ambayo imetoa chanjo kikamilifu kwa karibu asilimia 40 ya wakaazi wake dhidi ya maradhi ya Covid-19 kufikia mwishoni mwa mwaka 2021. Hivi sasa, zaidi ya asilimia 49 ya wakaazi karibu milioni 13 wa Rwanda wamepatiwa dozi mbili za chanjo ya coronana zaidi ya asilimia 61 wamepata dozi moja.

Lakini baadhi ya raia wa Rwanda wanasema idadi hiyo inawezekana tu kwasababu ya nguvu wanayotumia viongozi wa mitaa na polisi. DW ilizungumza na baadhi yao ambao wanadai kulazimishwa kuchanjwa. Kwa hofu ya kufuatiliwa, waliamua kutotaja majina yao.

Mwanaume mmoja kutoka wilaya ya Muhanga, katika jimbo la kusini la Rwanda, aliieleza DW kwamba alifungwa kamba ili aweze tu kuchanjwa. Anaendelea kusimulia hivi, "majira ya saa 10 alfajiri, kiongozi wetu wa mtaa aligonga hodi. Nilidhani ni wezi kwasababu nilikuwa nimelala. Kulikuwa na watu watatu wamesimama mlangoni kwangu, waliniamuru niende ofisini na nilikabidhiwa kwa afisa wa usalama na kuelezwa kuwa nitachanjwa bila ya ridhaa yangu".

Afrika Ruanda Kigali Corona Impfung
Wananchi wakiendelea na zoezi la chanjo RwandaPicha: Cyril Ndegeya/ Xinhua News Agency/picture alliance

Mwanaume huyo anakumbuka kwamba alilazimishwa kuketi chini ya jua hadi jioni alipopatiwa chanjo. Kulingana na maelezo yake polisi watano na maafisa wengine sita wa kiraia walikuwa wamemzingira hadi alipochanjwa kwa nguvu.

Majadiliano yafanyika kujenga kiwanda cha chanjo ya Covid Rwanda Baadhi ya watu walitaja tahadhari kutoka kwa viongozi wao wa dini kama sababu inayowafanya wasichanjwe. Waumini wa kanisa la Pentekoste, waliokataa kuchanjwa wanadai kwamba walishikiliwa na maafisa wa usalama kwa takribani wiki moja wakishawishiwa kupigwa chanjo. "Tulikataa kabisa kupigwa chanjo na badala yake tukawaomba askari na polisi kutupiga risasi au kutuzamisha hadi tufe. Tulipinga, lakini walisema hatutowapiga risasi", mwanamume mmoja aliimbia DW.

Mwanaume mwingine kutoka wilaya ya Rwamagana katika jimbo la mashariki alikimbia nyumbani kwake yeye na mkewe wakati maafisa walipojaribu kuwalazimisha kuchanjwa "nilikuwa naugua malaria na ninatumia dawa. niliwaomba wasinichanje na waliposisitiza nilikimbia nyumbani". Kwa mujibu wake, majirani zake wengi walilazimishwa kupigwa chanjo. Hata hivyo DW haikuweza kuthibitisha shuhuda hizo zinazotolewa na baadhi ya raia.

Afrika Ruanda Kigali Corona Impfung
Wananchi wakisubiri kupatiwa chanjo RwandaPicha: Cyril Ndegeya/ Xinhua News Agency/picture alliance

Lakini shirika moja ambalo ni mwamvuli wa mashirika ya haki za binadamu Rwanda la CLADHO, lilisema katika taarifa yake kwamba limepata ripoti za watu kulazimishwa chanjo. "CLADHO iko katika mchakato wa kufanya uchunguzi wa kupata picha kamili juu ya hali hiyo" alisema mkurugenzi wake Emmanuel Safari ambaye anadai vitendo hivyo ni kinyume na haki za binadamu.

DW iliyatafuta mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu Amnesty International na Human Rights Watch na yote yalisema kwa hivi sasa hayana taarifa juu ya ripoti za watu kulazimishwa chanjo chini Rwanda. Mbaali na hilo DW pia ilijaribu kuwasiliana na wizara ya afya ya Rwanda na ofisi ya waziri Mkuu lakini hapakuwa na majibu kutoka mamlaka hizo.

Christopher Nkusi ambaye ni meya wa wilaya ya Ngororero, ametupilia mbali madai hayo ndani ya mkoa wake akisema ni ya uongo. "Wale wanaopinga huwa wanaelimishwa na kisha kupatiwa chanjo baadae kwasababu hata sasa tunao watu wengi ambao bado hawajachanjwa. Bado tuko katika mchakato wa kuwashawishi. Sina taarifa za mtu yeyote aliyelazimishwa kuchanjwa.

Madai ya watu kulazimishwa kwa kutumia nguvu au shinikizo la kisaikolojia yamekuwa yakisambaa kwa wiki kadhaa sasa. Mnamo mwezi Desemba kulikuwa na vidio iliyosambaa katika mitandao ya kijamii nchini humo, ilimuonyesha mzee mmoja aliyesikika akisema katika kinyarwanda kuwa hataki kupigwa sindano au kuchanjwa. Baadae kulikuwa na picha iliyosambaa na ilimwonyesha mwanaume aliyeketi chini wakati mwingine aliyevalia sare za kijeshi akimshika mabega na mtu mwingine wa tatu akimchoma sindano.