Askari wa Kongo waliokimbia mapigano kushitakiwa
10 Februari 2025Taarifa iliyotolewa Jumapili na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi ilisema kuwa askari hao pia wanashitakiwa kwa vurugu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji na uporaji.
Soma: Hali bado ni tete nchini Kongo, Katibu Mkuu wa UN Guterres akiomba amani
Wanajeshi 75 wanaokabiliwa na kesi walikamatwa kwa kukimbia mapigano baada ya kushikiliwa kwa mji wa Nyabibwe. Wanatuhumiwa kwa ubakaji, mauaji, uporaji na uasi, ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi imelieleza shirika la habari la Reuters.
Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukaji mkubwa ikiwemo unyongaji, ubakaji wa magenge na utumwa wa kingono kufuatia msako mkubwa wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari ambao ulipelekea kutekwa kwa mji mkubwa wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iligundua kwamba wapiganaji wa M23 na askari wa serikali pamoja na wanamgambo wanaounga mkono serikali wote wanahusika. Kongo bado haijatoa tamko kuhusu ripoti hiyo kuhusiana na vikosi vyake lakini imeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukajiinaodai unafanywa na M23 na Rwanda.
Rwanda, ambayo inakanusha kuunga mkono kundi la M23, imekataa jukumu lolote. Waasi wa M23 hawajajibu maombi ya kutoa maoni yake. Licha ya tangazo la upande mmoja la usitishaji mapigano, waasi hao wameendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu.
Chanzo cha mashirika ya kiraia huko Kavumu, mji ulio kilomita 35 kaskazini mwa Bukavu na ambako kunapatikana uwanja wa ndege wa jiji hilo, kilisema wanajeshi waliotoroka wamewaua watu 10, wakiwemo saba waliokuwa wameketi kwenye baa siku ya Ijumaa jioni.
"Vitendo vya uporaji vilivyofanywa na askari wetu wasio na udhibiti ambao wamekimbia mbele ya adui bado vinarekodiwa," alisema kiongozi mwingine wa mashirika ya kiraia katika eneo hilo, Leonidas Tabaro.
Soma: Majeshi ya Kongo, Burundi yashirikiana kuwazuia waasi wa M23 kusonga mbele mashariki mwa Kongo
Msemaji wa jeshi la mkoa huo Nestor Mavudisa alisema askari hao wakorofi wataadhibiwa na kuwataka wananchi kuwa watulivu.
Mwishoni mwa juma kumeripotiwa utulivu kiasi, ingawa mapigano yaliripotiwa katika mbuga ya kitaifa karibu kilomita 30 kutoka Bukavu, pamoja na kurushiana risasi za hapa na pale katika eneo hilo.
Katika hatua za kujaribu kuutatua mgogoro huo, viongozi wa Afrika walikutana mwishoni mwa juma katika mkutano wa kilelena kuzitaka pande zote kufanya mazungumzo ya moja kwa moja.
Serikali ya Kongo ilisema Jumapili kwamba imezingatia maamuzi yaliyopitishwa wakati wa mkutano huo.