1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Wanajeshi Ukraine waendeleza mapambano huko Soledar

13 Januari 2023

Ukraine imesema kuwa wanajeshi wake wangali wanapambana katika mji wa mashariki wa Soledar baada ya usiku wenye mapigano makali. Pande zote zimekumbwa na hasara kubwa katika mapambano ya kuwania udhibiti wa mji huo mdogo

https://p.dw.com/p/4M7Ka
Ukraine-Krieg | Kämpfe um Soledar
Picha: Libkos/AP/dpa/picture alliance

Ukraine imesema leo kuwa wanajeshi wake wangali wanapambana katika mji wa mashariki wa Soledar baada ya usiku wenye mapigano makali. Pande zote zimekumbwa na hasara kubwa katika mapambano ya kuwania udhibiti wa mji huo mdogo. Moscow inatafuta kile kinachoweza kuwa ni mafanikio yake ya kwanza makubwa kwenye uwanja wa mapambano baada ya kipindi cha nusu mwaka ambao askari wake wamelazimika kurudi nyuma. Kyiv inasema Urusi inaendelea kupeleka vikosi vyengine vya wanajeshi katika eneo hilo la Soledar, maarufu kwa uchimbaji chumvi. Soledar ipo katika mkoa wa kiviwanda wa Donestk ambao Urusi inalenga kuukamata. Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Hanna Malyar, amesema ilikuwa ni usiku wa moto katika eneo la Soledar ambako mapambano yanaendelea, akiita hii kuwa awamu ngumu ya vita hivyo lakini mwishowe watashinda.