1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Wanajeshi kadhaa wa Urusi wauawa Ukraine

Saleh Mwanamilongo
2 Januari 2023

Ukraine inasema imewauwa karibia wanajeshi 400 wa Urusi katika shambulio la kombora kwenye eneo linalokaliwa na wanajeshi wa Urusi la Donetsk.

https://p.dw.com/p/4LeKs
Ukraine Donezk | Angriff auf russische Militär-Unterkunft nahe Makiiwka
Picha: RIA Novosti/SNA/IMAGO

Katika taarifa muda mfupi uliopita, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wanajeshi wake 63 wameuliwa kufuatia shambulio la makombora manne. Taarifa hiyo inaelezea kuwa shambulio hilo lilisababisha mlipuko mkubwa kwenye kambi ya muda ya wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine. Bila kudai shambulio hilo, jeshi la Ukraine lilisema karibu wanajeshi 400 wa Urusi waliuawa huko Makiivka katika eneo linalodhibitiwa na Moscow la mkoa wa mashariki wa Donetsk.

Siku ya mwaka mpya, Urusi ilizidisha mashambulizi ya anga ya usiku kwenye miji ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na Kyiv. Hiyo inaashiria mabadiliko katika mbinu za Urusi baada ya miezi kadhaa. Baada ya kurusha makumi ya makombora mnamo Desemba 31, Urusi ilitumia makumi ya ndege zisizo na rubani za Shahed zilizotengenezwa na Iran mnamo Januari 1 na Januari 2. Lakini serikali ya Ukraine ilisema Jumatatu kuwa iliangusha ndege zisizo na rubani zote 39, zikiwemo 22 kwenye anga ya mji mkuu Kyiv.

Kyiv alisema mbinu hiyo mpya ni ishara ya kukata tamaa kwa Urusi kwani uwezo wa Ukraine wa kulinda anga yake ulikuwa umeimarika.

''Tunasimama kwa umoja''

Rais Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr ZelenskyPicha: AFP/Getty Images

Rais Volodymyr Zelenskiy aliwasifu raia wa Ukraine kwa kuonyesha mshikamano kwa wanajeshi wao na kusema Urusi haitofanikiwa kuisambaratisha Ukraine.

''Wanaogopa. Unaweza kuhisi. Na wana haki ya kuogopa. Kwa sababu watapoteza. Ndege zisizo na rubani, makombora, kila kitu kingine hakitawasaidia. Kwa sababu tunasimama kwa umoja. Wameunganishwa tu na hofu.''

Mkuu wa ofisi ya rais Zelensky Andriy Yermak alisema kwenye akaunti yake ya Telegram kuwa Urusi imekuwa ikijaribu kuharibu miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa miezi lakini imeshindwa kwa sababu Ukraine ilipata ulinzi bora.

Katika ujumbe mkali wa mkesha wa Mwaka Mpya uliorekodiwa mbele ya kikundi la watu waliovalia sare za kijeshi, rais Putin aliapa kutojisalimisha kamwe kwa Urusi kwa nchi za Magharibi, kwa kile alichosema kuwa ni  hatua ya nchi hizo ya kuitumia Ukraine kama chombo ilikuisambaratisha Urusi.

Msaada wa Umoja wa Ulaya

Rais wa Almashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amethibitisha uungaji mkono wa muda mrefu wa umoha huo kwa Ukraine katika kuzima mashambulizi ya Urusi. EU inatoa msaada wa jenereta, malazi na mabasi ya shule kwa Ukraine msimu huu wa baridi na hivi karibuni itaanza kutoa bilioni Euro biliaoni 18 kama kifurushi cha usaidizi wa kifedha kwa serikali ya Kyiv.