1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 8 wahukumiwa kifo na Mahakama ya kijeshi DRC

28 Desemba 2022

Wanajeshi wanane na raia mmoja wamehukumiwa kifo na Mahakama Kuu ya Kijeshi ya Bunia DRC baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya raia wawili wa China ambao walikuwa pia wafanyabiashara wa dhahabu.

https://p.dw.com/p/4LUBy
Symbolbild | Justiz
Picha: fikmik/YAY Images/IMAGO

Miongoni mwa waliohukumiwa ni Kanali Mukalenga Tendeko na Kayumba Sumahili ambao inaaminika walipanga shambulio Machi 17, 2022 dhidi ya msafara uliyotokea mgodini na uliyokuwa ukisafirisha dhahabu na dola 6, 000 pesa taslimu katika kijiji cha Nderemi eneo la Irumu katika Jimbo la Ituri.

Kulingana na mwendesha mashtaka, silaha zilizotumiwa katika uhalifu huo ziliuzwa na kundi la kisiasa na kidini la CODECO ambalo katika miaka ya hivi karibuni, limelaumiwa kwa mauaji ya idadi kubwa ya raia huko Ituri.

Hukumu ya kifo hutolewa mara kwa mara nchini Kongo lakini utekelezaji wake kiuhalisia hubadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela.