1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yamtaka Blinken kutetea haki katika safari yake Afrika

8 Agosti 2022

Shirika la kimataifa la kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limesema leo kuwa ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken barani Afrika lazima itoe kipaumbele kwa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/4FGZk
Antony Blinken besucht Südafrika
Picha: Andrew Harnik/AFP

Rai hiyo Human Rights Watch imeitoa wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken akianza safari yake barani Afrika, ambayo miongoni mwa mambo mengine ni kukabiliana na ushawishi wa Urusi barani humo. Ziara hiyo ameianzai nchini Afrika Kusini, na baadaye atakwenda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Human Rights Watch imesema ziara hiyo inakuja huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kwamba kundi la waasi la M23, linaendelea kupokea uungwaji mkono wa Rwanda katika mashambulizi yake dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusisitiza kuwa ziara hiyo inatoa fursa ya kulaani mashambulizi hayo ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita lakini pia kuangazia kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu na ukandamizaji dhidi ya wapinzani unaofanywa na Rwanda.

Wasiwasi huo wa Human Rights Watch una msingi katika ripoti iliyovuja ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa, ambayo ilisema ina ushahidi wa kutsha kuwa Rwanda imewasaidia waasi wa M23 katika mashambulizi yao. Rwanda lakini imeikanusha ripoti hiyo ikisema ni uongo mtupu.

Nchini Afrika Kusini Blinken atatoa hotuba muhimu katika Chuom Kikuu cha Pretoria, ambako atabainisha sera ya Marekani kuhusiana na Afrika ya kusini mwa Jangwa la Sahara.

-ape, afpe