1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanahabari Tanzania wataka kubadilishwa sheria ya utangazaji

George Njogopa12 Agosti 2022

Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania limeanza majadiliano na maafisa wa serikali nchini humo kwa ajili ya kufikia makubaliano ya namna ya kuifanyia marekebisho sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/4FTCp
Tansania Debatte über Media gegen Fake News
Picha: DW/E. Boniphace

Sheria hiyo ambayo tangu kupitishwa kwake inatajwa kuwa mwiba kutokana na baadhi ya vipengele vyake kubana uhuru wa vyombo vya habari, huenda ikafanyiwa marekebisho katika miezi ya hivi karibuni na hilo linadhihirika baada ya pande zote mbili yaani jukwaa la wahariri na serikali kupiga hatua katika majadiliano yao ya awali.

Majadiliano hayo yaliyowahusisha baadhi ya viongozi wa jukwaa la wahariri na maafisa wa serikali kutoka Wizara ya habari, mawasialiano na teknolojia ya habari pamoja na ofisi ya mwanasheria wa serikali yameridhia baadhi ya vipengele kwenye sheria hiyo vifanyiwe marekebisho.

Kulingana na mwenyekiti wa jukwaa hilo la wahariri, Deudatus Balile pande hizo mbili zimeafikiana kuviondoa baadhi ya vipengele ambavyo kulingana na muktadha wa sasa, havina mantiki yoyote kuendelea kuwepo ndani ya sheria hiyo.

Hata hivyo, Balile anasema pande hizo bado zimeshindwa kuafikiana katika baadhi ya vipenegele na kwa maana hiyo katika duru lingine la majadiliano masuala hayo yanajadiliwa tena.

Sheria yenye utata ?

Sheria ya huduma kwa vyombo vya habari iliyopitishwa wakati wa utawala uliopita ni miongoni mwa sheria ambazo zinatajwa kuzidisha mbinyo kwa waandishi wa habari kuwa na uhuru katika kutekeleza majumu yao.

Waandishi wengi wa habari wanasema wanajikuta katika wakati mgumu kutekeleza majukumu yao kutokana na sheria hiyo, lakini sasa wanaanza kuonyesha sura za tabasamu kutokana na hatua hiyo iliyoanzishwa kama anavyosema mmoja wa mwandishi huyu, Kelvin Matandiko.

Moja ya mambo yanayotajwa kuwa ya kupigiwa mfano wakati ilipochukua hatua za oungozi Rais Samia Suluhu Hassan ni kuashiria nia ya kutaka uhuru wa vyombo vya habari, akizingulia televisheni za mtandao na magazeti kadhaa ambayo leseni zake zilifutiliwa mbali.