1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi watekwa tena Nigeria

17 Februari 2021

Serikali ya Nigeria imesema watu waliojihami kwa bunduki, wameivamia shule moja katikati mwa nchi hiyo, na kumuua mwanafunzi mmoja pamoja na kuwateka nyara wanafunzi wengine kadhaa na jamaa zao pamoja na walimu.

https://p.dw.com/p/3pUu3
Symbolbild Entführung Schüler Nigeria
Picha: Sunday Alamba/picture-alliance/AP

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akizungumzia utekaji nyara wa hivi karibuni katika shule moja nchini humo, ameviamuru vikosi vya usalama kuratibu operesheni za kuwaokoa wanafunzi waliotekwa. Rais Buhari aliye na miaka 78 amelaani kitendo hicho na kutaka wanafunzi hao warejeshwe nyumbani haraka iwezekanavyo 

Watu zaidi ya 40 walichukuliwa mateka na majambazi hao, waliovalia mavazi ya kijeshi walipokivamia chuo cha serikali cha sayansi katika mji wa Kagara katika jimbo la Niger kabla ya kuwapeleka watu hao katika msitu mmoja uliokuwa karibu.

Mamia ya wanafunzi walichukuliwa

Maafisa wa serikali wamesema baadhi ya wanafunzi walitoroka na hadi sasa haijajulikana ni wanafunzi wangapi hasa waliotekwa nyara. Kwa sasa vikosi vya usalama vikisaidiana na vile vya angani vinaendelea  kuwatafuta majambazi hao ikiwa ni harakati za kuwaokoa waliotekwa.

Symbolbild Entführung Schüler Nigeria
Viatu vya wanafunzi waliotekwa shuleniPicha: Sunday Alamba/picture-alliance/AP

Ripoti kutoka kwa serikali zinasema mamia ya wanafunzi walichukuliwa kutoka katika vyumba vyao shuleni humo huku Msemaji wa jimbo la Niger Muhammad Sani Idris, amesema takriban wanafunzi 650 walikuwepo shuleni wakati wa shambulio. Makundi ya majambazi waliojihami kwa bunduki Kaskazini Magharibi na katikati mwa Nigeria wameimarisha mashambulizi yao katika miaka ya hivi karibuni, kwa kuwateka watu kwa ajili ya kupata fidia pamoja na kuwabaka wanawake na wasichana.

Utakumbuka miezi miwili iliyopita zaidi ya wanafunzi 300 walitekwa nyara kutoka katika shule moja mjini Kankara katika jimbo la Katsina. Baadaye wanafunzi hao wa kiume waliotekwa walirejeshwa nyumbani baada ya majadiliano kati ya serikali na watekaji. Kisa hicho hata hivyo kilizua hisia kali kote duniani.

Serikali ya Nigeria inapaswa kutangaza hali ya dharura

Utekaji nyara wa mara kwa mara unaofanywa na magengeya majambazi Kaksazini Magharibi mwa Nigeria ni changamoto moja kubwa iliopo katika taifa hilo lililo na idadi kubwa ya watu barani Afrika, ambako maafisa wa usalama wanapambana na makundiiya wapiganaji walio na misimamo mikali ya kidini katika eneo la Kaskazini Mashariki, mapigano ya kikabila na uharamia upande wa Kusini.

Symbolbild Entführung Schüler Nigeria
Viatu vya wanafunzi waliotekwa shuleniPicha: Sunday Alamba/picture-alliance/AP

Idayat Hassan mkuregenzi wa taasisi ya Idayat inayoshughulikia masuala ya demokrasia na maendeleo amesema srikali ya Nigeria inapaswa kutangaza hali ya dharura kutokana na ukosefu wa usalama pamoja na kuhakikishwa shule zinalindwa ipasavyo la sivyo utekaji nyara wa wanafunzi utaendelea.