1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa Syria wafikia 60,000

Admin.WagnerD3 Januari 2013

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu waliouwawa nchini Syria imeongezeka hadi kufikia 60,000 katika mapigano ambayo mpaka sasa haijafahamika kikomo chake.

https://p.dw.com/p/17CqP
UN High Commissioner for Human Rights Navi Pillay delivers her speech at the Human Rights Council side-event on Syria at the United Nations in Geneva, Switzerland, Monday, Sept. 10, 2012. U.N. Secretary-General Ban Ki-moon urged before the world’s foremost human rights body to keep up the pressure on major powers to end the civil war in Syria and outbreak of human abuses there. (Foto:Anja Niedringhaus/AP/dapd)
Navi PillayPicha: AP

Katika mapigano ya hivi karibuni, idadi kubwa ya watu ilipoteza maisha katika viunga vya jiji la Damascus, pale ambapo makombora ya anga ya jeshi la Syria yalipovurumishwa katika kituo kimoja cha mafuta. Mwanaharakati mmoja katika eneo hilo, Abuu Saed, alinukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) akisema alishuhudia miili ya watu 30 ikiwa imeungua na mingine kusambaratika vipande vipande. Tukio hilo lilitokea katika eneo la Muleiha, kitongoji ambacho vikosi vya serikali vilitekeleza operesheni yao dhidi ya waasi.

Kwa upande wa kaskazini, waasi walianzisha operesheni nyingine kubwa ya mashambulizi ya kukidhibiti kiwanja cha ndege na kwamba walijigamba kufanikiwa katika zoezi hilo kwa kusema wameteketeza ndege pamoja na helikopta.

View of buildings damaged by what activists said were missiles fired by a Syrian Air Force fighter jet loyal to President Bashar al-Assad in Binsh near Idlib January 2, 2013. REUTERS/Muhammad Najdet Qadour/Shaam News Network/Handout (SYRIA - Tags: CONFLICT) FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS IMAGE HAS BEEN SUPPLIED BY A THIRD PARTY. IT IS DISTRIBUTED, EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS
Hali ilivyo katika mji wa IdlibPicha: Reuters

Idadi ya vifo inatisha

IAkizungumza mjini Geneva, Uswisi mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navy Pillay, amesema watafiti kutoka katika vyanzo saba tofauti vya utafiti, ambao umefanyika kwa miezi mitano umebaini watu 59,648 wameuwawa nchini Syria kati ya Machi 15, mwaka 2011 na Novemba 30, mwaka 2012.

Mkuu huyo mwenye dhamana na ustawi wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa aliendelea kusema kuwa athari za vita hivyo zimekuwa kubwa zaidi ya vile ilivyotarajiwa jambo ambalo linashtusha sana. Amesema kwa namna inavyoonekana hakuna unafuu utakaotokea katika vitendo vya mauwaji na kwamba wanaweza kukadiria kwamba katika siku za mwezi uliopita sambamba na mwanzoni mwa mwezi huu, idadi ya watu waliouwawa huenda ikaongezeka zaidi na kuvuka kiwango hicho cha sasa.

Kwa mujibu wa takwimu hizi mpya hakuna ufafanuzi kiwango au idadi ya waoliuwawa hasa ni watu wa aina gani, waasi, majeshi ya serikali au raia wa kawaida na wala kuonesha kwamba wakati gani idadi ya vifo ilizidi au kupungua.

Msemaji wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Rupert Colivelle alisema "Nafikiri idaidi hii inashangaza, ni zaidi ya kila mmoja alivyokuwa akifikiria. Tumeona picha jinsi maeneo yalivyovurugika huko Allepo, Homs na maeneo ya Damascus, kwa hivyo haiwezi kushangaza. Lakini hii inadhihirisha kushindwa jumuiya ya kimataifa ikiwemo sisi Umoja wa Mataifa, kuufikisha kikomo mgogoro huu."

Waangalizi wasema hali mbaya

Awali Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria lenye mfungamano na upande wa waasi lilisema idadi ya watu waliokufa imefikia 45,000 tangu kuanza kwa vuguvugu la kumng'oa madarakani rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, inagwa nalo pia lilisema idadi halisi huenda ikaongezeka zaidi.

Vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo pia ni mgogoro uliosababisha mauwaji zaidi vilizuka wakati wa vuguvugu la nchi za kiarabu mwaka 2011 ambapo hivi sasa umeendelea na kuwa kama mgogoro wa kimadhehebu katika taifa hilo.

Waasi ambao wengi wao kutoka upande wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni walio wengi, wanapambana na jeshi la Assad pamoja na vikosi vingine vya usalama ambao wengi wao ni Washia waliochanganyika na watu wa madhehebu ya Alawi. Wengi wa jamii ya madhehebu hayo na mengine madogo madogo wanahofia kwamba rais Assad akianguka kunaweza kukatokea vitendo vya kulipiziana visasi.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri:Josephat Charo