1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinda amani wa UN watuhumiwa kutelekeza watoto Congo

13 Januari 2023

Baadhi ya wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, wanaomaliza muda wa utumishi wao na kuondoka, wanaacha nyuma yao watoto kadhaa waliowatelekeza.

https://p.dw.com/p/4M9i2
Demokratische Republik Kongo | MONUSCO Mission | Goma
Picha: Olivia Acland/REUTERS

Shirika la habari la AFP lilikutana na wanawake kadhaa mkoani Kivu Kusini wanaodai kuzaa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Ingawa wanawake hawa hawaripoti kutendewa ukatili wa kijinsia, lakini wengine walikuwa na umri kati ya miaka 14 na 15 walipokutana na askari hawa waliowa hadaa kwa ahadi za ndoa, pesa au zawadi ndogondogo.

Sasa wanajeshi hao wameondoka na kuwaacha na watoto wa kuwalea peke yao. Wanacho kumbana nacho kwenye jamii yao ni unyanyapaa. Mmoja wao ni Masika, mwanamke mwenye umri wa miaka 29. Anaeleza kuwa hana mume na wala wanaume hawamtaki tena, kwa sababu amezaa mtoto na mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa.

DRK Nach Überfall auf Konvoi von Luca Attanasio
Askari wa MONUSCOPicha: Alexis Huguet/Getty Images/AFP

Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15 tu, na alikuwa akiuza karanga karibu na duka la mjomba wake, lililokuwa karibu na kambi ya kijeshi ya "Adi-Kivu". Ndipo alipokutana na askari huyo wa Umoja wa Mataifa, ambaye alimfuatilia kwa miezi sita, akawa akimpa pesa mara kwa mara. Anasema mwanzoni alikataa kwa kuwa aliogopa, lakini hatimaye akamkubalia.

Lakini wakati Masika alipogundua kuwa ni mjamzito, mlinzi huyo wa amani kutoka  Afrika Kusini alikuwa tayari ameshaondoka Kongo, na namba yake ya simu haikuwa ikitumika tena. Alijifungua, akamzaa mtoto Catherine, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 14 na anasoma Shule ya Kavumu.

MONUSCO inalipa ada na kununua vifaa vya shule. Catherine ni kama watoto wengine wa jirani na anakua kwa kasi, lakini tatizo pekee ni kwamba mara nyingi mtoto humuuliza mama yake baba yake yuko wapi, naye anakosa jibu.

Sifa, mwenye umri wa miaka 27, pia anasema alikuwa na mahusiano na mlinda amani wa Afrika Kusini, ambaye jina lake halijui, wakati akiwa bado hajafikisha umri wa miaka 15. Wakati huo alikuwa akifanya kazi katika mkahawa mdogo katika uwanja wa ndege wa Kavumu na huku akienda shule, ambayo alilazimika kuachana nayo alipopata ujauzito. Binti yake, Neema, haendi shule. Tafauti na Masika, Sifa hakuchukua hatua muhimu kwa wakati, na hakuwekwa kwenye orodha ya wanufaika.   

DR Kongo | MONUSCO | Unrühen
Askari wa MONUSCOPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Zawadi Bazilyane, mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la wanawake, na kiungo kati ya MONUSCO na watu hawa walioathirika na suala hilo, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wamebaini ndani ya shirika lao watoto 11, ambao mama zao wanasema walizaliwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka mataifa mbalimbali. Anasema wawili walikufa, tisa walibaki, na wote ni vijana.

Bazilyane anasema walipata shida kuweka pamoja mafaili, kwa sababu mara nyingi wanawake hawa hawana utambulisho halisi wa baba wa watoto wao. Na kwa hiyo, vipimo vya damu haviwezekani au ni vigumu sana kufanya. Lakini wanakusanya ushahidi, kutoka kwa msafara, kutoka kwa wakuu wa vijiji na kadhalika.

MONUSCO hulipa ada na vifaa vya shule, wakati akina mama wanajifunza biashara, kama vile kushona ama kusuka vikapu. Wengine hupokea mbuzi kwa ajili ya mifugo. Ilipoulizwa, MONUSCO ilisema, inahakikisha kuwa madai yote ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya walinda amani, yanashughulikiwa mara moja. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa waathirika na watoto wao wanapata msaada unaofaa.

Tangu mwaka 2013, kulingana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa, hakuna kesi zilizoripotiwa katika eneo la Kavumu na vijiji vya karibu dhidi ya walinda amani. Matumaini ni kwamba hii inatokana na ushirikiano kati ya MONUSCO kwa upande mmoja, na mashirika yasiyo ya kiserikali na mitandao ya kijamii, inayofanya kazi ya kuhamasisha watu dhidi ya unyanyasaji wa kingono, kwa upande mwingine.