1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa majeshi Afrika Mashariki wakutana Goma

8 Juni 2022

Wakuu wa majeshi wa mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa majadiliano ya kuunda kikosi cha pamoja kurejesha usalama kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4CP6H
Kongo I Flucht vor  M23-Rebellen
Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Mkutano huo wa Jumanne (Juni 7) ulifanyika katika mji mkuu wa kibiashara wa mashariki mwa Kongo, Goma, bila ya ushiriki wa Rwanda, ambapo taarifa iliyotolewa inasema wakuu hao wa kijeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walijadili hatua za awali za muundo wa kikosi hicho.

Ingawa haikuelezewa undani kuhusu lini na nani watakuwemko katika kikosi chenyewe, lakini sehemu ya taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo ilisema kikosi hicho "kitasaidia kudhibiti na itakapobidi kupambana na vikosi vya maadui mashariki mwa Kongo." 

Mkutano wa jana ulifanyika wakati Rais Yoweri Museveni wa Uganda akihutubia taifa na ambapo pia alizungumzia kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inao uwezo wa kutumia njia za kisiasa kutatua changamoto za usalama nchini Kongo. 

Museveni alisema msimamo wake wa kutumia majadiliano unahusiana hasa na makundi yasiyo ya kigaidi na yenye silaha mashariki mwa Kongo, lakini pia mlango uko wazi kwa hata makundi ya kigaidi, katika kile kinachoonekana kuwalenga waasi wa nchi yake wanaofanya zao ndani ya Kongo, kundi la ADF-Nalu.

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame

Uganda imetuma wanajeshi wake kwenye eneo hilo kupambana na kundi hilo kwa mualiko wa serikali ya Kinshasa.

Tshisekedi ailaumu Rwanda

Siku ya Jumapili akiwa ziarani katika taifa jirani la Jamhuri ya Kongo, Rais Felix Tshisekedialisema hakuna mashaka yoyote kwamba "Rwanda inaunga mkono uasi" ndani ya nchi yake, ingawa alisisitiza kuwa angelitumia njia za amani kulimaliza suala hilo na Kigali. 

Kongo - taifa kubwa zaidi kwa eneo na lenye wakaazi milioni 90 - ilijiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Machi, wakati sehemu yake kubwa ya mashariki ikiwa inakabiliwa na mapigano na ukatili wa kinyama unaofanywa dhidi ya raia na makundi yenye silaha.

Eneo hilo tete limegeuzwa kuwa uwanja wa vita vya siasa za kikanda likizikutanisha Uganda, Rwanda na Burundi, miongoni mwa mataifa mengine. 

Serikali mjini Kinshasa mara zote imekuwa ikiilaumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi yenye silaha ndani ya ardhi yake kwa maslahi yake yenyewe.

Inaihusisha moja kwa moja Rwanda na kuibuka tena kwa kundi la M23 mwezi uliopita, tuhuma ambazo zinakanushwa vikali na serikali mjini Kigali.