1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima wafurahia marufuku ya nyama ya punda, Kenya

Admin.WagnerD25 Februari 2020

Maelfu ya wakulima ambao ni wafugaji wa punda nchini Kenya wameelezea afueni kufuatia marufuku iliyotangazwa na waziri wa kilimo wa nchi hiyo dhidi ya machinjio ya punda nchini kote Kenya.

https://p.dw.com/p/3YPCX
Italien | Esel auf Bergwiese im Trentino
Picha: Imago Images/CHROMORANGE/H. Eder

Mashirika ya kutetea haki za wafugaji hao, wanaeleza kuwa kinyume na dhana kwamba hatua hiyo itaathiri uchumi wa taifa, sasa sekta hiyo itaweza kuimarika. 

Na mara tu alipotoa amri hiyo waziri wa kilimo Peter Munya, wafugaji wa punda waliokuwa wamepiga kambi mbele ya afisi yake jijini Nairobi kushinikiza ombi lao dhidi ya unyanyasaji wanaosema unaletewa na biashara ya machinjio ya punda nchini, walivuta pumzi ya ahueni. Isack Laisa, mfugaji wa punda ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa wakulima walio wafugaji wa punda nchini Kenya, anasema  wamekuwa wakihangaika tangu machinjio ya kwanza ya punda yalipofunguliwa mwaka 2016.

Esel Farm und Museum in Montenegro
Kenya ina machinjio manne ya punda na kuna soko kubwa la nyama yakePicha: DW/R. Kračković

Kenya ina machinjio manne ya punda yaliyoko maeneo ya Machakos, Naivasha, Mogotio na Turkana. China na Vietnam ndio soko kubwa zaidi la bidhaa zitokanazo na wanyama hao. Wataalam wanahoji kuwa biashara hiyo haiwezi kujimudu kwa kuwa punda hawazaani kwa haraka ndio maana wasambazaji punda kwa machinjio waligeukia wizi ili kudumisha biashara yao. Inaripotiwa kati ya punda 80-100 wamekuwa wakiibiwa kila mwezi.

Dr Raphael Kinoti, mkurugenzi mkuu katika shirika la Farming Systems Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la mashirika yanayofanya utetezi wa mnyama punda nchini Kenya, anakana kwamba uchumi wa taifa utaathirika kutokana na marufuku hiyo. Akiunukuu utafiti, Kinoti anasema biashara ya machinjio ya punda imekuwa ikimfaidi mfanyabiashara tu, kwa kuwa watu 457 walioajiriwa hapo na wakulima waliokuwa wakisambaza punda walikuwa wakipata malipo duni.

Kinoti anaeleza kuwa sasa wanalenga kuwaimarisha zaidi ya wakulima laki 2 nchini Kenya ambao ni wafugaji wa punda.

Mwaka uliopita ripoti iliyotolewa na shirika la Africa Network for Animal Welfare ilieleza kuwa kufikia mwaka 2023 punda watakuwa wametoweka nchini Kenya, hali iliyoambatanishwa na hatua ya kuanisha nyama ya punda na farasi kama chakula.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.