1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi katika kambi za Magharibi mwa Tanzania kupata misaada ya dharura ya chakula

Epiphania Buzizi12 Agosti 2005

Umoja wa Ulaya umetoa msaada wa Euro milioni saba kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wanaokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula katika kambi mbali mbali za wakimbizi nchini Tanzania.

https://p.dw.com/p/CHfI
Makambi ya wakimbizi nchini Tanzania
Makambi ya wakimbizi nchini TanzaniaPicha: AP

Msaada huo ambao ni sawa na kiasi cha dola za Kimarekani milioni 8.7,umetolewa katika kipindi kisichotimia mwezi mmoja , baada ya shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kuonya kwamba wakimbizi wapatao laki nne nchini Tanzania walikuwa katika hali ya kukubwa na njaa.

Mkurugenzi mkaazi wa shirika la mpango wa chakula Duniani tawi la Tanzania, Patrick Buckley amesema kwamba msaada huo umekuja kwa wakati unaofaa, kwani upungufu wa misaada ya kifedha ulisababisha maafisa wa shirika hilo kugawa misaada kidogo ya chakula kwa wakimbizi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Amesema msaada uliotolewa na Umoja wa Ulaya utawawezesha maafisa wa WFP kutoka misaada kwa siku chache zijazo.

Mwezi uliopita ,shirika la mpango wa chakula Duniani pamoja na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, yalitoa mwito kwa wahisani kutoa misaada ya dharura ya nyongeza kiasi cha dola za kimarekani milioni 5 kwa ajili ya chakula cha wakimbizi katika kambi 12 za wakimbizi Magharibi mwa Tanzania.

Walisema bila ya hivo, mashirika hayo yangelazimika kupunguza misaada ya chakula kwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.

Maafisa wa shirika la kuhudumia wakimbizi, wanasema kwamba hatua ya kupunguza misaada ya chakula ilisababisha kuwepo kwa masikilizano magodo katika baadhi ya familia za wakimbizi hao. Wakimbizi wengine walilazimika kutafuta ajira nje ya makambi yao, ambapo mara nyingine walikabiliana na wahalifu waliohatarisha usalama wao.

Shirika la kuhudumia wakimbizi liliripoti kwamba linahangaishwa mno na vitendo vya kuwaonea wanawake wakimbizi kwenye makambi hayo Magharibi mwa Tanzania.Matatizo ya chakula yalichangia kuzuka kwa magonjwa mbali mbali yakiwemo utapia mlo.

Wakati awakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na baadhi ya wakimbizi wa Rwanda waking’ang’ania kubaki makambini na kuomba misaada ya chakula, licha ya hali ya salama makwao,wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi wameanza kurejea nchini mwao.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi wanarejea kwao nbaada ya kuwa na imani na hali ya usalama nchini humo.

Msemaji awa shirika hilo Jennifer Pagonis amebainisha kuwa wiki iliyopita UNHCR iliwasaidia wakimbizi 4200 wa Burundi kurejea makawao wakitokea Rwanda na Congo Kinshasa.

Maafisa wa UNHCR wanatarajia kwamba jumla ya wakimbizi watakaohiari kurejea makwao mwezi huu itafikia elfu 20, ongezeko la mara sita kuliko ilivyokuwa mwezi June na Julai mwaka huu.

Wakimbizi wamewaambia mafisa wa UNHCR kwamba uchaguzi wa madiwani uliofanyika nchini Burundi mwezi June , umewapa matuamaini ya kurejea kwa amani nchini humo, na haja ya kurejea makwao baada ya kipindi cha miaka tisa ya kuishi uhamishoni.

Hata hivyo Bi.Pagonis amesema kuwa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa ambalo limekuwa likiwasaidia raia wa Burundi kurejea kwao kwa hiari,halijaanza rasmi zoezi la kuwarejesha makwao wakimbizi hao.

Amebainisha kuwa bado kuna hofu juu ya uslama wa wakimbizi hao hususan wakati huu kunaporipotiwa mapigano ya hapa na pale kati ya majeshi ya serikali ya Burundi na waasi katika mji wa Bujumbura licha ya usitishwaji mapigano na mazungumzo ya amani nchini humo.