1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi 3,000 DRC wajificha bondeni kufuatia mashambulizi

Mitima Delachance28 Aprili 2021

Wakimbimbizi zaidi ya 3000 wa ndani nchini DRC wamejihifadhi katika vijiji vya bonde la mto Ruzizi tangu mwanzoni mwa juma, kufuatia mapambano makali yanayo ripotiwa kati ya makundi yenye silaha.

https://p.dw.com/p/3sg1G
Symbolbild Weltbevölkerungsbericht Frauen
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Baadhi ya wakimbizi hao wa kabila la Banyamulenge wamekimbilia vijiji vya bonde la mto Ruzizi tangu mwanzoni mwa juma, kufuatia mapambano makali yanayo ripotiwa na vijiji vyao kuchomwa moto ndani ya milima ya wilaya ya Uvira.

Hali ya usalama inazidi kuzorota katika nyanda za wilaya ya Uvira ambapo mapambano ya kila mara yanaripotiwa kati ya muungano wa wanamgambo wa kabila la banyamulenge wanaoitwa Gumino na Twirwaneho na muungano wa wanamgambo Mai-Mai kutoka makabila mengine, pande hizo zote zikilaumiana kusaidiwa na waasi toka nchi za Rwanda na Burundi.

soma pia Kenya kutuma wanajeshi DRC kupambana na ugaidi

Mapigano hayo yanayoendelea kati ya vikundi hivyo vyenye silaha yamesababisha pia uharibifu wa mazao na kuchomwa kwa vijiji kadhaa.

Waliokimbia mapigano haya kwa sasa wanaishi katika hali duni bila msaada wowote haswa ndani ya vijiji vya Bwegera, Lemera na hata pia Kamanyola. 

Jeshi la DRC limesema halitaegemea upande wowote katika kusaka vikundi hivyo vyote vyenye silaha
Jeshi la DRC limesema halitaegemea upande wowote katika kusaka vikundi hivyo vyote vyenye silahaPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Viongozi wa vijiji vilivyowahifadhi wakimbizi hao wanahofia pia hali ya kiusalama, njaa na ufukara. Endapo hakutachukuliwa hatua za haraka, wengi wao watakuwa katika hatari ya kupoteza maisha yao kutokana na magonjwa, na mazingira magumu.

Marekani yapiga marufuku makundi mawili ya DRC na Msumbiji

Lucien Sogoti Rusimbi ambaye ni kiongozi wa jumuiya ya vijiji vya Kakamba katika wilaya ya Uvira, ameionya serikali ya Congo kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha usalama wa wakaazi hao.

Katika taarifa moja siku ya Jumanne, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika wilaya za Fizi na Uvira lililaumu machafuko hayo kwa mizozo ya kikabila iliodumu kwa muda mrefu katika wilaya hizo inayo sababishwa kila mara na wizi wa mifugo, ubakaji na mauaji, huku kila kundi lenye silaha likidai kulinda usalama wa raia wa kabila lake.

Jeshi limesema kwamba halitaegemea upande wowote katika kusaka vikundi hivyo vyote vyenye silaha vya ndani na vya kigeni vinavyotatiza usalama wa eneo hilo.