1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi 2,000 wa Burundi waanza safari ya kurudi kwao

Lubega Emmanuel21 Septemba 2021

Wizara ya majanga nchini Uganda imethibitisha kuwa zaidi ya wakimbizi 2,000 raia wa Burundi wameanza safari ya kurudi kwao wakiitikia wito wa rais wa nchi hiyo aliyewahakikishia mapokezi ya amani na usalama wao. Sikiliza ripoti ya mwandishi wetu Lubega Emmanuel kutoka Kampala.

https://p.dw.com/p/40bT5

Miongoni mwa wakimbizi hao ni wanasiasa wa upinzani ambao wameieleza DW kuwa wana imani sasa kuna mazingira ya amani ya kisiasa na wamekubali kufanya mazungumzo na serikali wakiwa nchini kwao.

Juhudi zinazofanywa na mashirika ya kibinadamu pamoja na serikali za Uganda na Burundi  kuwashawishi wakimbizi kutoka nchi hiyo zinazidi kuzaa matunda.

Aidha  kufuatia tamko la hima la mara kwa mara la Rais Evariste Ndayishimiye, wakimbizi hao wa Burundi wamekubali kurudi nyumbani kwa hiari.

Kuanzia siku ya Jumatatu, raia zaidi ya 2,000 wameanza safari za kwenda Burundi wakitokea Uganda ambako baadhi wameishi tangu mwaka 2006. Idadi nyingine ni ile iliyokuja mwaka 2015 baada ya mzozo wa kisiasa kuibuka. 

Waziri wa Majanga Hilary Onek, ameeleza kuwa kwa ushirikiano na mashirika kama vile la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR pamoja na serikali za Afrika Mashariki, wakimbizi hao wamesaidiwa kurudi kwao kwa kutumia ndege na njia ya barabara.

Jean- Bosco Ndayikengurukiye, mkimbizi wa kisiasa kutoka Burundi aliyekimbilia Uganda mwaka 2015.
Jean- Bosco Ndayikengurukiye, mkimbizi wa kisiasa kutoka Burundi aliyekimbilia Uganda mwaka 2015.Picha: Lubega Emmanuel/DW

Miongoni mwa wakimbizi ambao wanarudi Burundi ni viongozi wa kisiasa waliokimbilia Uganda mwaka 2015 wakipinga hatua ya aliyekuwa Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi kinyume na matarajio kuwa angeachia madaraka.

Jean- Bosco Ndayikengurukiye ambaye ni miongoni mwa wanachama wa ndani ya chama tawala cha CNDD-FDD waliopinga azma hiyo ya Nkurunziza mwaka 2015 ni mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu katika upinzani ambaye ana imani kuwa sasa mazingira ya kisiasa Burundi ni mazuri kwa wao kufanya mazungumzo na kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.

Wakiwa nchini Uganda, raia mbalimbali wa Burundi hasa vijana wameshiriki masomo na mafunzo ambavyo ni muhimu kwao kuanza tena maisha mapya nchini kwao.