1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wagawika kuhusu pendekezo la kuzuia "Mitumba' ya nje

Wakio Mbogho, DW, Nakuru9 Juni 2022

Wakenya wamegawanyika kuhusu kauli ya mgombea urais Raila Odinga kupiga marufuku biashara ya uuzaji wa nguo kuukuu zilizoagizwa nchini humo maarufu kama mitumba.

https://p.dw.com/p/4CSyD
Kenia Nairobi Gikombaa Markt
Picha: DW/B. Maranga

Ingawa Odinga ametoa hili kama suluhu la kufufua kampuni za kutengeza nguo zilizoangamizwa na mitumba, wapinzani wake wanamshtumu kuwa ana njama ya kuua sekta inayoajiri mamilioni ya Wakenya. Lakini ni zipi athari za biashara hii kwa uchumi wa taifa? 

Kauli ya kinara wa azimio la umoja Raila Odinga alipozindua manifesto yake kwamba ana mpango wa kufufua viwanda vya nguo vilivyoangamia na pia kubuni namna wafanyibiashara wa mitumba watakavyojumuishwa, imeibua mdahalo mkubwa kwenye vyombo ya habari, mitandaoni na mitaani,  wapinzani wake kutoka muungano wa Kenya Kwanza wakiichukua fursa hiyo kumkosoa kwa kuwadhalilisha wafanyibiashara wadogo.

Viongozi wanaojulikana kuwa wafuasi sugu wa muungano wa Kenya Kwanza walionekana kwenye picha na video wakinunua mitumba sokoni, huku wengine wakiipigia debe biashara hii mtandaoni.

Wapinzani wa Odinga kutoka muungano wa Kenya Kwanza watumia pendekezo lake kuimarisha sekta ya viwanda vya nguo ili kukuza biashara za nguo bora kutoka Kenya kumkosoa kwa kuwadhalilisha wafanyibiashara wadogo wa nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka ughaibuni..
Wapinzani wa Odinga kutoka muungano wa Kenya Kwanza watumia pendekezo lake kuimarisha sekta ya viwanda vya nguo ili kukuza biashara za nguo bora kutoka Kenya kumkosoa kwa kuwadhalilisha wafanyibiashara wadogo wa nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka ughaibuni..Picha: Raila Odinga press Team

Lakini, ni muhimu kuzingatia kwamba Raila Odinga alikuwa ameyatoa matamshi hayo siku chache baada ya mgombea Urais wa muungano wa Kenya Kwanza naibu Rais Wiliam Ruto kuyasema haya, kwenye mkutano wa kisiasa huko Kamukunji.

Mitazamo ya wachambuzi

Wachambuzi wanasema, wazo muhimu la kutathmini hatma ya biashara ya mitumba limepotea kwenye mabishano haya ya kisiasa. Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui amesema uchumi wa Kenya unaelekea pabaya na hii ni mojawapo ya suluhu.

Wafanyibiashara wawataka viongozi kutoingiza siasa kwenye sekta ya mitumba.
Wafanyibiashara wawataka viongozi kutoingiza siasa kwenye sekta ya mitumba.Picha: Monicah Mwagi/REUTERS

Jitihada za serikali ya Kenya kufufua kiwanda cha pamba, ambayo ilikuwa msingi wa biashara ya nguo nchini Kenya katika miaka ya 70 na 80 zimekuwa zikisuasua. Kibarua sasa ni kwa serikali ijayo kung'amua namna wanavyoweza kuimarisha viwanda vya nguo nchini, bila kuua biashara maarufu ya mitumba.

Wafanyibiashara wanawataka viongozi kutoingiza siasa kwenye sekta ya mitumba kwani inawapa riziki ya kila siku na ni kitega uchumi kwa mamilioni ya Wakenya.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.