1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya 32 wafungwa jela na mahakama ya kijeshi Uganda

13 Aprili 2023

Mahakama ya jeshi nchini Uganda imewahukumu raia thelathini na wawili wa Kenya vifungo vya miaka 20 jela kila mmoja kwa kupatikana na silaha kinyume na sheria.

https://p.dw.com/p/4Q18t
Brandstiftungen in Cabo Delgado
Picha: DW

Mahakama iliyofanya kikao kanda ya Karamoja kaskazini mashakiriki mwa nchi hiyo ilitoa adhabu hiyo kutokana na hatia ya wafugaji hao wa jamii ya Turkana kupatikana na bunduki na risasi. 

Kundi hilo ni miongoni mwa washukiwa waliokamatwa tarehe nane mwezi huu katika maficho yao wakiwa na bunduki 31 na risasi 751.

Hii ni kwa mujibu wa operesheni inayoendelea  eneo hilo kukamata silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria.

Hapo awali, watu wa jamii ya Karamoja walikuwa wamewasilisha malalamiko kuhusiana na kucheleweshwa kwa kesi hiyo kwani mshukiwa anapaswa kufikishwa mahakamani katika muda wa saa 48 baada ya kukamatwa.

Jamii za wafugaji wa kuhamahama eneo hilo ambalo ni makutano ya mataifa manne, Sudan kusini, Ethiopia, Kenya na Uganda zina uhuru wa kuvuka mipaka na kuingia nchi jirani iwapo kuna uhaba wa malisho nchini kwao.

Hata hivyo ni hatia kwao kumiliki sihala kinyume na sheria kwani zinaelezewa kuwa chanzo cha ukosefu wa usalama na pia vitendo vya wizi wa mifugo miongoni mwa jamii hizo na majirani zao.