1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani watafuta kazi nchi za ngámbo

P.Martin1 Agosti 2006

Tangu miaka kadhaa,idadi ya Wajerumani wanaohamia nchi za kigeni imeendelea kuongezeka.Mwaka huu hesabu hiyo imevunja rekodi:Wajerumani 145,000 wameihama nchi yao.Hiyo ni idadi kubwa kabisa tangu miaka 50 ya nyuma.

https://p.dw.com/p/CHms

Theluthi mbili ya Wajerumani wanaohamia nchi za kigeni hufanya hivyo kwa sababu ya ujuzi wa kazi na mara nyingi kwa vile hakuna njia nyingine katika soko la ajira.Si wengi wanaoondoka Ujerumani kwa hiyari,kwa hivyo baada ya miaka michache hurejea tena nyumbani.

Wengine wakiondoka Ujerumani kukimbia ukosefu wa ajira,wapo wale wanaozidi kuwa na kazi.Kwa mfano kwenye kituo kikuu cha kutoa kazi nchi za kigeni(ZAV) hakuna anaeweza kutamka kuwa kuna ukosefu wa kazi.Wataalamu wa kila aina huenda katika kituo hicho kutafuta kazi na kujaribu bahati zao katika nchi za kigeni.Kituo hicho, mwaka jana peke yake kiliwapatia kazi Wajerumani elfu 13 katika nchi za ngámbo.Nafasi nyingi za kazi ni za mafundistadi na wataalamu wa upishi,lakini hata wahandisi wana nafasi nzuri ya kupata kazi.

Kituo cha ZAV huwapa watu wazima,wasio na ajira uwezo wa mwisho wa kupata kazi.Kwani kinyume na soko la ajira la Ujerumani,nchini Uswissi na Uholanzi kwa mfano,ujuzi wa kazi unathaminiwa zaidi kuliko elimu ya kisasa.Kwa hivyo takriban asili mia 40 ya watu wanaopatiwa kazi na kituo cha ZAV ni wenye umri uliopindukia miaka 40.Kama ilivyokuwa mwaka jana,wengi huhamia nchi za Ulaya.Zaidi ya robo tatu ya wahamiaji huenda nchi za jirani wakiwa na matumaini ya kurejea Ujerumani.Nchi zinazowavutia wahamiaji wa Kijerumani nje ya Ulaya ni Kanada na Australia.

Azma ya wahamiaji wengi ni kupata ujuzi katika nchi za kigeni kwa matumani kuwa watakaporejea nyumbani watakuwa na nafasi bora zaidi za kupata ajira.Kwa mfano Daniel Lambart alikuwa na mawazo kama hayo.Baada ya kumaliza masomo yake ya usanifu majengo alipata kazi kwa mwaka mmoja tu katika ofisi ya wasanifu majengo.Akieleza kwa nini yeye kama wenzake wengi aliamua kutafuta kazi katika nchi ya kigeni,amesema:

“Niliona kuwa soko la ajira halikuweza kunipa kile nilichokitaka,kwa hivyo nilijaribu bahati yangu katika nchi ya Ulaya.Lakini hata huko sijafanikiwa.Baadae niliangukia idara ya misaada ya maendeleo ya Ujerumani na nikapeleka maombi yangu na utaratibu wa kuniajiri ulikwenda kwa haraka.”

Kila mwaka idara hiyo,hupeleka wataalamu katika nchi zinazoendelea.Hasa ni mafundistadi,wakulima na wataalamu wa elimu wanaohitajiwa.Lakini hata wasanifu majengo wanaweza kuajiriwa:na Lambart akapata kazi nchini Togo.Kinyume na mpango wake wa mwanzo wa kutaka kubakia Ulaya,safari hii,bila shaka,ilikuwa ya ujasiri na kusisimua.

Msanifu majengo Lambart ameeleza hivi maarifa yake ya kufanya kazi nchi ya ngambo:

“Sina majuto kuhusu wakati huo,kwani nimekusanya maarifa mengi ninayoweza kutumia katika maisha yangu ya leo.”