1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubaguzi bado ni tatizo Ujerumani

7 Agosti 2018

Zaidi ya nusu ya Wajerumani walioshiriki kura ya maoni ya kila mwezi wanauweka ubaguzi wa rangi katika kundi la maovu makuu katika jamii.

https://p.dw.com/p/32jG0
Berlin AfD-Demonstration
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Utafiti wa Infratest Dimap wa mwezi Agosti unaonyesha kwamba asilimia 64 ya Wajerumani walioulizwa kuhusiana na ubaguzi wa rangi walisema kwamba ni "tatizo kubwa sana" au ni "tatizo kubwa" huku asilimia 35 wakisema ubaguzi wa rangi ni tatizo dogo tu huku wengine wakisema si tatizo kabisa.

Maoni haya ndivyo yalivyo katika ulingo mzima wa kisiasa isipokuwa kwa wafuasi wa chama cha AfD ambao asilimia 37 tu yao ndio wanaouona ubaguzi wa rangi kama tatizo kubwa sana au tatizo kubwa. Asilimia 77 ya wafuasi wa chama cha wanamazingira cha Kijani pamoja na chama cha Social Democratic wanasema ubaguzi ni tatizo.

Suala lililoshangaza kiasi cha haja katika utafiti huu ni kwamba asilimia 68 ya watu walio na chimbuko la uhamiaji ndio walioona kwamba ubaguzi wa rangi ni tatizo huku asilimia 63 ya watu wasio na na chimbuko hilo wakiwa wanaona ni tatizo kubwa.

Matokeo hayo hayakushangaza sana pale Wajerumani wa mirengo tofauti ya kisiasa walipoulizwa iwapo wahamiaji wa madaraja mawili - wale waliowasili hivi karibuni na wale waliowasili miongo kadhaa iliyopita - walikuwa wametangamana katika jamii, ambapo asilimia 62 ya walioulizwa walisema suala la kutangamana limefanikiwa ila idadi kubwa ya wafuasi wa AfD walikana hilo.

Wapigaji kura wa chama cha Social Democrat kulingana na utafiti huo wameonekana kuwakubali zaidi wahamiaji wa zamani huku asilimia 77 yao wakisema utangamano umefanikiwa kwa kundi hilo la wahamiaji.

Infografik Deutschlandtrend Rassismus in Deutschland EN
Matokeo ya uchunguzi wa maoni kuhusu ubaguzi Ujerumani

Walipoulizwa ni mambo gani ambayo ni muhimu kwao asilimia 97 ya watu walisema ni sera zinazoathiri utoaji wa huduma ya afya na hata huduma kwa wazee ni mambo muhimu mno. Haya yalifuatiwa na hofu kuhusiana na malipo ya uzeeni ambapo asilimia 95 ndio waliokubali na asilimia 90 wakasema wanajali sana kulingana kulindwa kutokana na uhalifu.

Serikali haiwaridhishi walio wengi

Wajerumani lakini wameonekana kutoridhishwa na serikali yao kwani serikali mpya ya Kansela Angela Merkel ambayo ni yake ya nne tangu mwaka 2005 imepata alama za chini mno katika masuala ya kubuni nafasi bora za kuishi huku asilimia 77 wakisema hawajaridhishwa kabisa au hawajaridhishwa. Asilimia 16 ya watu walisema kwamba wameridhishwa na serikali katika suala hilo la makaazi huku ikiwa hakuna aliyesema kwamba ameridhika kikamilifu katika jambo hilo.

Kutokana na takwimu hizi si jambo la kushangaza kuona kwamba serikali ya muungano ya wahafidhina na wasocial demokrat bado inaendelea kupata uungwaji mkono mdogo kwenye kura za maoni. Walipoulizwa ni chama kipi ambacho wangekipigia kura iwapo uchaguzi ungefanywa hivi karibuni ni asilimia 29 tu ya walioulizwa waliosema kwamba watapigia vyama ndugu CDUna CSU. Asilimia 18 ya watu walisema kwamba watapigia kura chama cha Social Demoratic. Hii inaonyesha kwamba serikali ya sasa ya muungano inaweza kukosa wingi wa viti bungeni.

Chama cha AfD bila shaka kinaendelea kunufaika kutokana na mgogoro wa ndani kwa ndani wa vyama vya kihafidhina kuhusiana na sera ya uhamiaji kwani kwa sasa chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kushoto kimepata alama moja zaidi na asilimia 17 wanasema watakipigia kura iwapo uchaguzi ungefanyika hivi karibuni. Chama cha wanamazingira cha kijani kimepata alama moja zaidi pia na asilimia 15 ndio waliosema watakipigia kura, hiyo ikiwa ndiyo asilimia kubwa zaidi ya uungwaji mkono waliyopata tangu mwaka 2013.

Mwandishi: Jacob Safari/DW

Mhariri: Mohammed Khelef