1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu washerehekea sikukuu ya Eid ul Adha

28 Juni 2023

Waislamu wanasherehekea sikukuu ya Eid ul Adha inayohitimisha kipindi cha hajj kote ulimwenguni. Ibada ya Hajj ni moja kati ya nguzo ya Kiislamu ambayo kila mwenye uwezo anapaswa kufanya angalau mara moja maishani mwake.

https://p.dw.com/p/4TAi8
Indien Islam Opferfest Eid al-Adha
Waislamu wakiswali salah maalum ya Eid kuadhimisha kukamilika kwa ibada ya Hajj.Picha: NARINDER NANU/AFP/Getty Images

Nchini Kenya, takwimu zinaonyesha kuwa waislamu alfu 4 wameshiriki ibada ya hajj mjini Makka mwaka huu nchini Saudi Arabia.

Sherehe za Eid Ul Adha zina uzito mkubwa kwani ni sunna ya mtume Ibrahim kutii amri ya kumtoa kafara mwanawe wa kiume Ismail, ambayo ni ishara ya imani kubwa kwa Mwenyezi Mungu.

Eid Ul Adha ni hitimisho la hajj inayofanyika kila mwaka mjini Mecca, Saudi Arabia ulio mtukufu kwa waislamu.

Kulingana na dini ya Kiislamu, kila mwenye uwezo anatakiwa kwenda hajj angalau mara moja maishani mwake.

Eid al-Fitr in Nigeria
Waislamu nchini Nigeria wakipiga picha baada ya kuswali swala maalum ya EidPicha: Adeyinka Yusuf/AA/picture alliance

Kabla ya kuelekea Mecca kwa Hajj, waziri wa ulinzi wa Kenya Aden Duale aliwatakia heri mahujaji wote walipokuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA.

Wasioweza kwenda hajj husalia majumbani mwao na kufanya sala maalum na ibada ya kuchinja mnyama kama vile ng'ombe, mbuzi, kondoo au ngamia kisha kugawana nyama hiyo na majirani na watu wasiojiweza.

Ili kuwapa nafasi waislamu kushiriki ibada hii muhimu, waziri wa usalama wa taifa nchini Kenya Kithure Kindiki ameitangaza siku hii kuwa ya mapumziko kupitia gazeti rasmi la serikali.

Sherehe za Eid Ul Adha zinafanyika wakati ambapo Kenya inakabliana na kipindi kigumu cha kiuchumi kwani gharama za maisha zimepanda.

Kadhalika kodi zimeongezwa ili kufadhili bajeti ya kwanza ya serikali ya rais William Ruto ya shilingi trilioni 3.6.

Kwenye ujumbe wake maalum,kiongozi wa taifa amewatakia waislamu kheyr na baraka pamoja na kudumisha misingi ya sikukuu ya Eid Ul Adha ya kujitolea, imani na kumtii Mwenyezi Mungu.

Sikukuu ya Eid Ul Adha hufanyika katika siku ya kumi ya mwezi wa Dhul Hijjah ambao ni wa 12 na wa mwisho kwenye kalenda ya kiislamu.

Dhul hijja ni moja ya kati ya miezi minne mitukufu katika kalenda ya Kiislamu.