1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi kuendelea kuwaunga mkono Wapalestina

30 Mei 2024

Waasi wa Houthi wakiendelea kuzishambulia meli kwenye Bahari ya Shamu wakidai kuwa ni ishara ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita vyao na Israel huko Gaza.

https://p.dw.com/p/4gSwO
Yemen | Waasi wa Houthi wakiandamana dhidi ya Marekani na Israel
Waasi wa Houthi wakiandamana huko Yemen dhidi ya Marekani na Israel: 29/01/2024Picha: Osamah Yahya/dpa/picture alliance

Kiongozi wa waasi wa Kihouthi kutoka Yemen ambao wanafadhiliwa na Iran Abdulmalik al-Houthi amesema hii leo kuwa wataendelea kwa kasi na ufanisi mkubwa harakati zao za kijeshi katika dhamira ya kuwaunga mkono Wapalestina katika  vita vyao na Israel huko Gaza.

Tangu mwezi Novemba, kundi hilo limekuwa likishambulia meli zenye mafungamano na Israel katika Bahari ya Shamu na hivyo kulazimisha shehena za mizigo kutumia njia nyengine ya mbali na iliyo ghali kwa wasafirishaji.

Wahouthi wametanua mashambulizi yao hadi kwenye Bahari ya Hindi na kusema watazilenga meli zozote zinazoelekea kwenye bandari za Israel katika Bahari ya Mediterania.

Israel yaendeleza mashambulizi huko Rafah

Mashambulizi ya Israel huko Gaza
Mashambulizi ya Israel huko Gaza: 13/05/2024Picha: Abdul Rahman Salama/Xinhua/IMAGO

Watu wasiopungua kumi na wawili ambao ni raia wameuawa hii leo huko Rafah huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza ambayo inadhibitiwa na Hamas iliyoorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya magharibi kama kundi la kigaidi.

Soma pia: Israel yaishambulia Rafah licha ya uamuzi wa ICJ

Mapigano yameripotiwa eneo la kati, kusini na hata kaskazini mwa Gaza lakini Israel haijatoa taarifa yoyote juu ya vifo hivyo vilivyoripotiwa huko Rafah, ambako kumekuwa kimbilio la mamia ya maelfu ya Wapalestina.

Israel imeendeleza operesheni yake huko Rafah licha ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kuamuru usitishwaji wa mapigano eneo hilo. Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amemsisitizia mwenzake wa Marekani Lloyd Austin kuhusu umuhimu wa kuendelea na operesheni huko Rafah kutokana na taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya mateka wameshikiliwa eneo hilo.

Kitisho cha njaa katika ukanda wa Gaza 

Gaza - Msaada wa chakula ukisubiriwa kutolewa kwa Wapalestina na Shirika la UNRWA
Msaada wa chakula ukisubiriwa kutolewa kwa Wapalestina na Shirika la UNRWA katika Ukanda wa GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Wakati vita vikiendelea, Gaza inakabiliwa na kitisho kinachoongezeka cha utapiamlo kutokana uwasilishaji wa misaada kupungua. Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kutokea baa la njaa eneo hilo.

Philippe Lazzarini, mkuu Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, ameitolea wito Israel kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya wafanyikazi na majengo ya UNRWA huko Gaza.

Soma pia: UNRWA yasema Wapalestina milioni moja wakimbia Rafah

Hii leo, serikali ya Slovenia imeidhinisha uamuzi wa kuitambua Palestina kama taifa huru. Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Robert Golob:

"Serikali ya Slovenia imeamua kutosubiri hadi Julai,  Tutaitambua Palestina Alhamisi hii kwa sababu tumekasirishwa na kile kinachotokea Rafah na Gaza. Tunataka huu uwe ujumbe wa wazi kwa ulimwengu mzima. Ni lazima tufanye kila liwezekanalo kutafuta suluhu na amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati."

Hata hivyo uamuzi huo unatakiwa mnamo siku zijazo kupitishwa na Bunge la Slovenia.

Vyanzo: Mashirika