1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti wasema hakuna kipya katika ripoti ya nyuklia

Abdu Said Mtullya18 Mei 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wazungumzia juu ya ripoti ya wataalamu kuhusu usalama wa vinu vya nyuklia nchini

https://p.dw.com/p/11IpF
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Nobert RöttgenPicha: picture-alliance/dpa

Jopo la wataalamu lililoteuliwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel limewasilisha ripoti juu ya usalama wa vinu vya nyuklia nchini Ujerumani. Wataalamu hao wamesema, vinu hivyo kwa jumla ni salama.

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya ripoti hiyo.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung anasema kwamba hamna jipya katika ripoti ya wataalamu hao. Anaeleza kuwa badala ya wataalamu hao kushauri wazo la kuvifunga kabisa , vinu vya nyuklia nchini Ujerumani, wametoa ripoti juu ya yale ambayo kila mdau anayajua kwa uhakika- kwa mfano wanasema vinu hivyo vya nyuklia hivimo katika hali ya kujihami kwa uhakika endapo inatokea ajali ya ndege na kuangukia kwenye vinu hivyo. Au ripoti inasema baadhi ya vinu havina uwezo kabisa wa kujihami dhidi ya ajali kama hizo.

Gazeti la Der neue Tag linasema ,ripoti iliyotolewa na wataalamu juu ya usalama wa vinu vya nyuklia, nchini Ujerumani siyo ya kuutuliza moyo. Gazeti hilo linaeleza kwamba kati ya vinu 17 vinne havimo katika hali ya kujihami dhidi ya ajali ya ndege na katika mazingira fulani lisingelikuwa tatizo kwa ndege kuingia katika vinu hivyo.

Ukweli sasa umedhihirika kwamba nishati ya nyuklia siyo salama na wala siyo ya bei nafuu. Bali ukweli uliopo ni kwamba, bei ya umeme ingelikuwa ya juu sana endapo, taratibu za usalama zinazostahili zingelichukuliwa.


Mhariri wa gazeti la Darmstädter Echo anasema kulingana na ripoti iliyowasilishwa na wataalamu,itakuwa vigumu kufikiria kwamba vinu vya nyuklia vitaendelea kutumika nchini Ujerumani.

Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linasema Ujerumani inahitaji sera mpya ya nishati. Linasema tofauti na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya watu nchini Ujerumani wanatambua kwamba nishati ya nyuklia siyo njia salama sana. Wajerumani wamebaini hayo kutokana na hatari zinazoandamana na matumizi ya nishati ya nyuklia. Kwa hiyo Ujerumani inahitaji mageuzi ya kimsingi katika sera ya nishati.

Sera hiyo lazima iwe na shabaha maalumu na ielekezwe katika kujenga mustakabal wenye uhakika. Hata hivyo anasema mhariri wa gazeti hilo kwamba hayo hayataweza kufanyika mara moja na wala hayataweza kutekelezwa bila ya gharama kubwa.

Gazeti la Westdeutsche linasema muda wa wiki sita uliotumika kufanya uchunguzi juu usalama wa vinu vya nyuklia ni mfupi. Hata hivyo gazeti linasema serikali imepita katika njia sahihi kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia . Lakini sasa kila mwanachi wa Ujerumani anayo haki ya kujua ni lini Ujerumani itaacha kutumia nishati ya nyuklia na vipi Ujerumani itaendelea kukidhi mahitaji ya nishati bila ya nyuklia ya nyuklia.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ Yusuf Saumu