1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji zaidi ya 900 wafa maji pwani ya Tunisia

27 Julai 2023

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia, Kamel Feki amesema walinzi wa pwani wa nchi yake wameipata miili 901 ya wahamiaji waliozama katika pwani yake kuanzia Januari Mosi hadi Julai 20 mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4USFq
Tunesische Küstenwache stoppt Schiff mit Migranten auf dem Weg nach Italien
Picha: Hasan Mrad/ZUMA/picture alliance

Feki ameliambia bunge la nchi yake kuwa miongoni mwa maiti hizo, 36 zilikuwa za raia wa Tunisia na 267 za wahamiaji wa kigeni, huku waliobakia bado uraia wao haujatambuliwa.

Tunisia imechukua nafasi ya Libya kama kituo kikuu cha kanda hiyo kwa watu wanaokimbia umasikini na mizozo Afrika na Mashariki ya Kati kwa matumaini ya kwenda Ulaya kupata maisha bora.

Soma zaidi: Mpango wa EU wa kuokoa uchumi wa Tunisia

Boti nyingi zenye wahamiaji zinaondoka kwenye pwani ya mji wa kusini wa Sfax.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa takribani wahamiaji 75,065 waliwasili nchini Italia baina ya Januari hadi katikati ya mwezi Julai mwaka huu, ikilinganishwa na wahamiaji 31,920 katika miezi sawa na hiyo kwa mwaka jana.

Zaidi ya nusu ya wahamiaji hao waliondokea nchini Tunisia.