1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wa Ureno

Lillian Urio15 Septemba 2005

Idadi ya wahamiaji ya Ureno imepanda sana katika miaka iliyopita. Wahamiaji wengi wanatokea nchi zilizo tawaliwa na Ureno wakati wa ukoloni na hawa jumuishwi ipasavyo na kuishia kuwa wageni miaka yao yote.

https://p.dw.com/p/CHel

Watu wengi wanaoishia kuitwa wageni ni watoto au wajukuu wa wale waliohamia Ureno, ingawa wao wamezaliwa nchini humo. Wazazi wao wengi walihamia kutoka nchi za Afrika zilizokuwa makoloni ya Ureno.

Hii ni kwa sababu kutokana na sheria ya Ureno mtu anakuwa na uraia wa nchi hiyo kama wazazi wake ni wazaliwa wa Ureno. Hivyo huwezi kupata uraia kwa kuzaliwa tu nchini humo.

Ndio maana kuna watu ambao maisha yao yote wameishi Ureno lakini serikali ya nchi hiyo inawahesabu kama, ni wananchi wa Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau, Msumbiji, Timor Mashariki na Sao Tome na Principe.

Wengine wanahesabika kama wananchi wa India kwa sababu mababu zao walitokea Goa, Diu na Daman, maeneo ambayo leo ni sehemu ya India,yaliyokuwa chini ya utawala wa Ureno hadi mwaka 1961. Wengi wao hawajawahi hata kufika kwenye nchi hizo.

Alcestina Tolentino kutoka shirikisho la watu kutoka Cape Verde anasema wanapigania sheria hiyo ibadilishwe.

“Kuwawezehsa wahamiaji kupata uraia ndiyo njia pekee ya kuwapatia haki sawa na Wareno. Sisi tunachopigania hasa ni kuwa na haki sawa.”

Jambo hili pia linawagusa wahamiaji kutoka Brazil, walioanza kuhamia kwa wingi Ureno katika miaka ya 80.

Sasa hivi kuna Wabrazil 120,000 wanaoishi Ureno na ndio kikundi kikubwa zaidi cha wahamiaji kutoka nchi yoyote humo. Na watoto wa wahamiaji hao, hata kama wamezaliwa Ureno, bado wanahesabika kama wageni.

Bwana Amarilio Mendoca, mwenye miaka 25, ambaye hivi karibuni alihitimu kutoka chuo kikuu cha Lisbon, ni mtoto wa wahamiaji kutoka Cape verde na analalamika kwamba yeye ni mgeni katika nchi aliyozaliwa na hata katika nchi waliozaliwa wazazi wake.

Akizungumza na shirika la habari la IPS amesema marafiki zake wa Kireno wanamwitwa mtu mweupe-mweusi, yaani mtu mweusi aliyeweza kujumuika katika jamii ya watu weupe. Lakini anasema akiwa nyumbani na familia yake basi anaongea ‘Creole’, mchanganyiko wa lugha za Kiafrika na Kireno, anasikiliza nyimbo kutoka Cape Verde na pia anakula chakula kutoka huko.

Anasema kwa mtazamo wake Ureno ni nyumbani kwake kwanza, ikifuatiwa na Cape Verde. Anakumbuka wakati alivyoitembelea Cape Verde na akawa anashangaa kwa sababu ni tofauti kabisa na Ureno.

Bwana Mendoca anasema watu wengi wanadhani kwamba kwa Waafrika wengi kama yeye waliozaliwa Ureno wanakuwa na tamaduni za Kiafrika zaidi kwa sababu wanafundishwa na familia zao.

Lakini anasema hiyo ni imani potofu kwa sababu alivyoitembelea Cape Verde aligundua kwamba yeye ni sawa na wageni wengine huko. Kwa hiyyo, kwa upande wake, cha muhimu zaidi ni sehemu mtu anapokuwa, na kwenda shule, kuanzia ya msingi hadi chuo kikuu.

Ingawa watoto na wajukuu wa wahamiaji kutoka Afrika wanajihisi zaidi ni Wareno, lakini bado jamii hiyo inawaona kama ni tofauti.

Bwana Mendoca anasema kuna sababu tofauti za kutowakubali kama Wareno, kuna wale ambao bado wanauchungu na vita vya ukombozi, vilivyofanyika kwenye nchi kadhaa za Kiafrika kuondokana na ukoloni wa Kireno.

Wareno wengine wanawahurumia na kuwaona kama wahanga wa Ukoloni wakatia wengine bado wanafikira kwamba Ureno inawamiliki, wakiwa na maana kwamba nchi zao za asili bado ziko chini ya Ureno.

Bi. Joacine Moreira mwanafunzi wa chuo, mwenye miaka 23, amekuwa akiishi mjini Lisbon nwa miaka 16. Bi. Moreira hakuzaliwa Ureno, bali Guinea-Bissau na amesema atakapomaliza masomo yake atarudi kwao, sababu kila siku anahisi yeye ni Mwafrika zaidi kuliko Mreno.

Ingawa amekuwa akiitembelea Guinea-Bissau wakati wa likizo Bi. Moreira anahofu kwamba atakaporudi kuishi na kufanya kazi huko, atakumbana na tatizo la utamaduni, sababu ameshazoea kuishi kama Mreno kwa miaka mingi.