1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji kutoka Zimbabwe wakumbana na matatizo

P.Martin8 Agosti 2006

Katika wilaya ya mpakani ya Limpopo,polisi wa Afrika ya Kusini mara kwa mara huwahujumu na huwadai pesa wahamiaji wa Ki-Zimbabwe, wanaoshindwa kuonyesha vyeti vya utambulisho au kuthibitisha kuwa wapo nchini kihalali.

https://p.dw.com/p/CHLO

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika linalotetea haki za binadamu “Human Rights Watch.”

Ripoti hiyo yenye kurasa 54 inaeleza vipi maafisa wanavyowakamata,kuwaweka kizuizini na kuwafukuza wahamiaji wa kigeni kwa njia ambazo zinakwenda kinyume na sheria za uhamiaji za Afrika ya Kusini.Ripoti hiyo pia inaeleza vipi wakulima wa biashara wanadharau sheria za kimsingi za ajira wanapowaajiri wageni.

Kwa mujibu wa makamu mkurugenzi wa Human Rights Watch,Georgette Gagnon,mara nyingi polisi wa Afrika Kusini huwatesa wafanyakazi wasio kuwa na vibali wanapowakamata.Na wanapongojea kurejeshwa makwao,hao wahamiaji hawawekwi mahala panapofaa wala hawapewi chakula cha kutosha katika vituo vya polisi.Wengine huzuiliwa zaidi ya siku 30,kinyume na sheria.

Vitendo hivyo vya maafisa wa Afrika ya Kusini vinakiuka sheria ya uhamiaji ya nchi hiyo pamoja na wajibu wake kwa mkataba wa kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa,uliotiwa saini na Afrika ya Kusini mwaka 1999.

Kwa mujibu wa Gagnon,wakulima hudharau kuwalipa mishahara kama inavyotakiwa kisheria.Hata wafanyakazi wenye vibali hulipwa mishahara iliyo midogo kuliko vile ilivyopangwa kisheria.Ripoti ya Human Rights Watch inaendelea kueleza kuwa sheria za uhamiaji na ajira za Afrika Kusini haziwalindi wageni vya kutosha.Kwa mfano sheria ya uhamiaji haiwaruhusu wafanyakazi wanaongojea kusafirishwa kwa sababu ya kutokuwa na vibali, kukusanya vitu na mishahara yao ambayo bado haijalipwa.Kisheria wafanyakazi wa kigeni wana haki ya kulipwa fidia,lakini mara nyingi hukabiliwa na vizingiti vingi.Shirika la Human Rights Watch limetoa mwito kwa serikali ya Afrika ya Kusini itekeleze sheria zake za ajira kwa kuongeza idadi ya wakaguzi wa ajira na kuanzisha mfumo utakaowawezesha waajiriwa kuwaripoti moja kwa moja waajiri wasiofuata sheria za ajira.Vile mashirika yasio ya kiserikali yapewe nafasi zaidi kusaidia kusimamia utaratibu wa ajira.

Licha ya matatizo hayo yote,Wazimbabwe wanaendeea kumiminika nchini Afrika ya Kusini ili kujiepusha na hali zinazozidi kuwa mbaya upande wa kisiasa na uchumi nchini mwao.Wengi hawana vyeti vya utambulisho na huingia Afrika ya Kusini kwa kuuvuka Mto Limpopo ulio mpakani.Inakadiriwa kuwa Wa-Zimbabwe hao wanaoishi nchini Afrika Kusini ni kati ya milioni 1.2 hadi milioni 3.