Wafusi wa Mursi wajiimarisha Misri
12 Agosti 2013Kitisho cha jeshi la polisi cha kuvunja mikusanyiko miwili ya wafuasi wa Chama cha Udugu wa Kiislamu, inafanya kuwepo kwa mashaka ya uwezekano wa kuzuka tena vurugu nchini Misri. Jeshi la taifa hilo mwezi uliopita lilimuondoa madarakani rais Mursi baada ya maandamano ya mamilioni ya watu kuupinga utawala wake.
Hatua ya sasa ya polisi, inaelezwa kuwa jeshi hilo linaweka milango wazi kabisa ya kutokea vurugu za makabiliano kati ya jeshi lenye kuungwa mkono na serikali na maelfu ya wafuasi wa rais alieondolewa madarakani, Mohammed Mursi.
Kauli ya waandamanaji
Waandamanaji tayari wamekwisha sema hawawezi kuondoka katika viwanja hivyo mpaka rais huyo aliendolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi Julai 3 mwaka huu arejeshwe madarakani.
Jitihada za mataifa ya magharibi kuumaliza mgogoro huo zimeshindwa. Mwisho wa juma, polisi imesema itadhibiti mkusanyiko wao wowote kwa kutumia maji ya kuwasha katika kuwasambaratisha. Lakini wanaharakati wa haki za binaadamu wameonya kwamba kuwaondoa kwa nguvu waandamanaji kutasababisha vitendo vya umwagikaji damu.
Kadhia ya maandamano ya Misri
Uongozi mpya wa Misri umesema maandamano hayo yanawatoa hofu raia wengine wa Misri, kusababisha vurugu zinazopelekea mauwaji na na kusababisha msongamano wa magari.
Viongozi katika mikusanyiko hio wamesema wametekeleza jukumu hilo kwa amani na wamevilalamikia vyombo vya usalama kwa kusababisha machafuko. Zaidi ya watu 250 wameuwawa tangu kuondolewa madarakani kwa Morsi.
Katika mkusanyiko mkubwa wa wafuasi hao mjini Cairo wachuuzi wa bidhaa ndogondogo wamesema wameuza idadi kubwa ya vifaa vya kujikinga na mashambulizi ya polisi kama vya kuziuia athari za mabomu ya machozi na vinginevyo. Wameweka vizuizi vilivyojengwa kwa saruji pamoja na mbao kwa ajili ya kuzuia magari lenye silaha ya vyombo vya usalama kuingia katika eneo hilo.
Kwa upande wao maafisa wa usalama wamesema wataweka vizuizi vya kuingia katika maeneo hayo ya maandamano kwa lengo la kuzuia yeyote kuingia, na kwamba mmoja kati ya maafisa hao alisema hatua hiyo ingalianza tu baada ya jua kuchomoza leo hii.
Lakini hata hivyo mpaka mapema asubuhi ya leo hakukuwa na ishara yoyote ya vikosi kuwasili katika maeneo hayo na kwamba serikali haijasema muda gani hasa itakwenda katika maeneo hayo ya waandamanaji.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri:Yusuf Saumu