1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa waadhimisha siku ya wanawake Kenya

8 Machi 2022

Wanawake waliofungwa katika gereza kuu jijini Nakuru huko Kenya, wameadhimisha siku ya wanawake ulimwenguni kwa njia ya kipekee kwa kuungana na wapendwa wao kupitia huduma ya mtandao.

https://p.dw.com/p/48BTv
Kenia Internationaler Frauentag Gefängnis
Picha: Wakio Mbogo/DW

Hafla hii iliibua hisia chungu nzima kwa wafungwa wa kike na jamaa zao, pale walipounganishwa na kuweza kuwasiliana na kuonana kupitia huduma ya mtandao.

Wengi wao hawajapata fursa ya kutembelewa na jamaa na marafiki tangia kipindi cha mkurupuko wa ugonjwa wa COVID 19 mwaka 2020.

soma Kenya yawaachilia huru wafungwa 14,000

Huduma hii ya mtandao iliyozinduliwa hii leo katika gereza kuu la wanawake jijini Nakuru inatekelezwa kwa ushirikiano na shirika linaloangazia afya ya kiakili, PDO, baada ya kutambua namna kina mama hawa walivyokuwa wanaathirika kutokana na maisha ya upweke, na changamoto kama vile umbali na hali ya kiuchumi iliyokuwa inawatatiza jamaa zao kufunga safari kuja kuwatembelea. Iregi Mwenja, mwanzilishi na mkurugenzi wa shirika hilo anaeleza.

“Kwa muda ambao tumeshirikiana na Kenya Prisons service, huduma ya kwanza ambayo tulianza ni kupeana ushauri nasaha kwa wafungwa, lakini baadaye tulielewa kwamba watu wanaoathirika katika mazingira ya jela, sio wafungwa pekeyake pia wafanyikazi wa magereza wanaathirika kwa sababu ni mazingira ambayo sio ya kawaida, na tukaanzisha mradi wa kuwalenga wafanyikazi. Wakati COVID 19 ilipoanza tulikosa nafasi ya kutangamana na wafungwa kwa sababu magereza yote yalifungwa. Na ndio tukakuja na huu mradi ambao unamuwezesha mfungwa kuonana moja kwa moja na mpendwa wake akiwa nyumbani.”

Mary Muhoro, Mkuu wa Gereza amesema mradi huu utakuwa wa manufaa sio tu kwa wafungwa bali kwa maafisa wanaouhudumu kwenye gereza hilo.

‘‘Unakuta siku ile tumeipanga kwa ajili yao kutembelewa, siku hiyo watu wao hawaonekani. Ikawa ni kazi ngumu. Tukaona sasa wafungwa wawe wanaonana na wapendwa wao bila vikwazo. Tuko na mpango wa kuendeleza mradi huu. Tukiufanya mara mbili kwa mwezi, hakuna mfungwa atakosa kuonana na jamaa zake. Mwishowe sisi tutakuwa na amani ya kuishi, wafanyikazi wawe na amani na wafungwa wawe na amani.“

Wadau waliofanikisha huduma hii wanalenga kuueneza mradi wenyewe ili kuweza kutumika kwenye magereza kote nchini, hivyo kuchangia kupunguza matatizo ya afya ya kiakili yanayoshuhudiwa kati ya wafungwa.

 

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.