1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyabiashara wadogo kuondolewa mitaani Dar es Salaam

Hawa Bihoga18 Oktoba 2021

Mamlaka imetoa muda wa mwisho wa siku kumi na mbili kwa wafanyabiashara wadogo walio katika maeneo yasioruhusiwa kuondoka na kwenda kwenye maeneo waliopangiwa.

https://p.dw.com/p/41o6r
Tansania Dar Es Salaam | Kariakoo Markt | Händler
Picha: Said Khamis/DW

Mamlaka ya mkoa wa Dar es salaam nchini Tanzania imetoa muda wa mwisho wa siku kumi na mbili kwa wafanyabiashara wadogo walio katika maeneo yasioruhusiwa kuondoka na kwenda kwenye maeneo waliopangiwa.

Hata hivyo uongozi wa machinga umeomba mamlaka hiyo ifikirie kuwabakisha katika maeneo yalio na muingiliano mkubwa wa watu kwani ndipo kwenye biashara.

Hawa Bihoga ametuandalia taarifa ifuatayo akiwa katika soko la kimataifa kariako, mjini Dar es salaam.

Mapema alfajiri katika jiji hili kuu la kibiashara, wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga wameamka wakiwa hawajui mustakabali wa biashara yao kwani leo ndio siku ya mwisho iliotolewa na mamalaka ya jiji hilo kupisha maeneo yote ambayo hayaruhusiwi kufanya biashara ikiwemo kando ya barabara na hata mbele ya maduka makubwa.

Katika soko la kimataifa kariakoo ambapo wafanyabiashara wadogo zaidi ya 1500 wapo hapa wakiendesha biashara na kuingiza pato kuzikimu familia, wanasema wanahitaji kuwa na uhakika wa biashara yao katika soko hilo linalohudumia zaidi ya watu 3000 kwa siku.

Majadiliano na uongozi wa wafanyabiashara

 Zaidi ya wafanyabiashara wadogo elfu tano wataathirika pakubwa na uamuzi wa mamlaka za miji
Zaidi ya wafanyabiashara wadogo elfu tano wataathirika pakubwa na uamuzi wa mamlaka za miji Picha: Said Khamis/DW

Itakumbukwa kwamba miaka kadhaa nyuma kundi hili halikuruhusiwa kuendesha shughuli zao katikati mwa miji na baadae serikali iliopita iliwatambua kwa kuwapatia vitambulisho kwa kuvinunua kwa shilingi 20000 hivyo kulifanya kundi hili kufanyakazi kwa uhuru.

Akizungumza na wafanyabiashara hao mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Amos Makala amesema, wanaingia katika majadiliano na uongozi wa wafanyabiashara hao huku akisisitiza kwamba serikali inawathamini kwa kuwapeleka maeneo ambayo yatafaa, ikiwa mipango ya muda mrefu ya mkoani ni kuliweka jiji hilo katika mpangilio wa kupigiwa mfano barani Afrika.

Ushauri wa rais Samia

Zaidi ya wafanyabiashara wadogo elfu tano wataathirika pakubwa na uamuzi wa mamlaka za miji kuwaondoa maeneo yaliokataliwa, hatua hii inaibua uongozi wa machinga Tanzania wakiisihi mamlaka kutekeleza amri hiyo kwa makubaliano kwani wafanyabiashara hao wanayo mikopo na kutegemewa na watoto kukidhi mahitaji yao. Makamo kwenyekiti wa machinga Tanzania.

Wakati tamko hilo la kuwahamisha wafanyabiashara hao likitoka katika miji mikubwa nchi nzima, Rais Samia Suluhu akiwa ziarani katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania, aliwasihi kundi hilo kushirikiana na mamlaka za miji katika kupanga miji kuwa kwenye muonekano wa kuridhisha.