Wachunguzi Korea Kusini wamhoji Rais Yoon Suk Yeol
15 Januari 2025
Rais wa Korea Kusini aliyepigiwa kura ya kutokuwa na imani, Yoon Suk Yeol, alikamatwa Jumatano na kuhojiwa kwa saa kadhaa na maafisa wa uchunguzi kuhusiana na tuhuma za uasi wa kijeshi, hatua ambayo imehitimisha mvutano wa wiki kadhaa kati yake na mamlaka.
Yoon, rais wa kwanza aliyepo madarakani kukamatwa katika historia ya Korea Kusini, alikamatwa kufuatia amri ya mahakama iliyotolewa baada ya wabunge kupiga kura ya kumwondoa madarakani kutokana na tangazo lake la muda mfupi la hali ya kijeshi mnamo Desemba 3. Baada ya kura hiyo, Yoon alijificha katika makazi yake yaliyoko juu ya kilima, akilindwa na walinzi wa rais waliokuwa wamezuia jaribio la awali la kumkamata.
Jumatano, baada ya zaidi ya maafisa 3,000 wa polisi kufika nyumbani kwake alfajiri kwa lengo la kumkamata, Yoon alijisalimisha mwenyewe katika ofisi za Uchunguzi wa Ufisadi kwa Maafisa Wakuu (CIO) kwa ajili ya kuhojiwa. "Nimeamua kushirikiana na uchunguzi wa CIO - licha ya kuwa ni uchunguzi haramu - ili kuepusha umwagaji damu usio wa lazima," Yoon alisema katika taarifa yake.
Wakati Yoon akiendelea kuhojiwa, mtu asiyejulikana mwenye umri wa miaka 60 alijaribu kujiua kwa kujichoma moto karibu na ofisi hizo, na kujeruhiwa vibaya.
Mamlaka zina saa 48 kuhoji Yoon kabla ya kuamua ikiwa watamwachia au wataomba kibali cha kumweka kizuizini kwa hadi siku 20. Hata hivyo, Yoon amekataa kuzungumza na pia hajakubali mahojiano yake kurekodiwa kwa video, jambo ambalo mamlaka zimeeleza kuwa haliwezi kueleweka.
Soma pia: Mkuu wa kitengo cha ulinzi wa rais Korea Kusini ajiuzulu
Katika wakati ambao mvutano wa kisiasa unaendelea, Mahakama ya Kikatiba inaendelea kutafakari iwapo itapitisha kura ya bunge ya kumwondoa Yoon madarakani moja kwa moja au imrudishe madarakani.
Huku Korea Kusini ikikumbwa na hali hii ya sintofahamu, Marekani imetoa tamko la kuunga mkono juhudi za Korea Kusini za kuheshimu katiba yao, huku Japan nayo ikifuatilia kwa karibu matukio hayo.
Wakati wa jaribio la kukamatwa kwake, maelfu ya watu walikusanyika mbele ya makazi ya rais wakishuhudia polisi wakivunja vizuizi na kuingia ndani, huku baadhi ya waandamanaji wanaomuunga mkono Yoon wakipambana na polisi.
Yoon ameendelea kushikilia msimamo wake kwamba alitangaza hali ya kijeshi kwa sababu ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi, ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo. Katika barua aliyoiandika kwa mkono na kuichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook, Yoon alisema amekuwa akionekana mjinga kwa sababu ya kukataa kufanya maafikiano.
Huku tafiti za maoni zikionyesha kuwa wananchi wengi wa Korea Kusini wanaunga mkono kumwondoa madarakani, mvutano huu wa kisiasa umechochea nguvu mpya miongoni mwa wafuasi wake, huku chama chake cha People Power Party (PPP) kikiimarika tena katika kura za maoni za hivi karibuni.