1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Uingereza wachagua kurefusha Brexit

Sekione Kitojo
15 Machi 2019

Wabunge wa Uingereza wamechukua msimamo kuhusu suala zima la kuongezwa muda wa kujitowa katika jumuiya hiyo badala ya tarehe 29 ya mwezi huu. 

https://p.dw.com/p/3F6Bh
UK Unterhaus lehnt zweites Brexit-Referendum ab
Picha: Reuters TV

Katika mkwamo  kuhusu Brexit , wanasiasa wa  Uingereza wamechagua  kuuchelewesha. Baada  ya  wiki za  mkwamo  wa kisiasa, bunge la  Uingereza  jana  lilipiga  kura  kutafuta kuahirisha kuondoka  kwa  nchi  hiyo  kutoka  Umoja  wa  Ulaya , hatua  ambayo huenda  ikaepusha  kujitoa  katika  hali  ya  mvurugiko katika  muda uliopangwa  wa  kujitoa  tarehe 29 Machi.

UK Unterhaus lehnt zweites Brexit-Referendum ab
Wabunge wa Uingereza baada ya kupiga kura kuhusu BrexitPicha: Reuters TV

Wakati  hatua  ya  kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya  maarufu  kama Brexit ikibakia  siku 15  na  hakuna  makubaliano  ya  kuvunja  ndoa ambayo  yameidhinishwa  hadi  sasa, baraza  la  wawakilishi  lilipiga kura  413 dhidi  ya  202  kuliomba  kundi  la  mataifa  ya  Umoja  wa Ulaya  kuahirisha hatua  ya  kujitoa  hadi  Juni  30. Matokeo  rasmi yalitangazwa  hapo  awali  kama  412 kwa 202, lakini  baadaye yalibadilishwa  na  kuwa  413  katika  orodha  rasmi  ya  upigaji kura.

Kura  hiyo  inampa  waziri  mkuu Theresa  May  muda  wa  kupumua kidogo, lakini  bado  ni kipigo  cha  kiongozi  ambaye  ametumia miaka  miwili  akiwaeleza  Waingereza  kwamba  wanajitoa  kutoka Umoja  wa  Ulaya  hapo  Machi 29.

UK Unterhaus für Brexit-Verschiebung und drittes Votum über Abkommen | Jeremy Corbyn
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uingereza Jeremy Korbyn akizungumza bungeni baada ya upigaji kuraPicha: Reuters TV

Hatima ya Uingereza sasa mikononi mwa EU

Nguvu  za  kuidhinisha  ama  kukataa  kurefushwa  kwa  hatua  hiyo imo  mikononi mwa  Umoja  wa Ulaya, ambao  umeashiria  kwamba utaruhusu ucheleweshaji  pale  tu  Uingereza  ama  inaidhinisha makubaliano  ya  kuachana ama  inafanya  mabadiliko katika kulishughulikia  suala  la  Brexit.

Katika  kichekesho  cha  kihistoria , karibu  miaka  mitatu baada  ya Uingereza  kupiga  kura  kujitoa  kutoka  Umoja  wa Ulaya , hali  yake ya  baadaye  hivi  sasa  imo  katika  mikono  ya  kundi  hilo  la mataifa.

May anatarajiwa  kuwaomba  viongozi  wa  Umoja  wa  Ulaya kurefusha  muda  wa  kujitoa  katika  mkutano  wa  viongozi  hao hapo  Machi 21 hadi 22  mjini  Brussels.

England, London: Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza akizungumza na wabunge la katika baraza la wawakilishiPicha: picture-alliance/House of Commons

Halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya  imesema  kuwa  Umoja  huo utatafakari  ombi  lolote, "ikitiliwa  maanani  sababu  za  na  kipindi cha  uwezekano  wa  kurefushwa."

May  amelazimika kutafakari  uchelewesho  wa  Brexit baada  ya wabunge  mara  mbili kukataa makubaliano  yake  ya  kuachana  na Umoja  wa  Ulaya  na  pia  kuondoa  uwezekano, kimsingi, kujitoa kutoka  katika  kundi  hilo  la  mataifa  bila  makubaliano. Kujitoa  bila ya  makubaliano  kutakuwa  na  maana  mparaganyiko  mkubwa  kwa upande  wa   makampuni na  biashara  pamoja  na  watu nchini Uingereza na  mataifa  27  yanayobakia  katika Umoja  huo.