1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge Ujerumani wajiuzulu baada ya kashfa ya barakoa

9 Machi 2021

Nchini Ujerumani wabunge wawili kutoka katika kambi ya vyama vinavyounda serikali wamelazimishwa kujiuzulu, baada ya kuzongwa na kashfa ya kunufaika na mauzo ya barakoa wakati huu wa janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3qNrd
Bundestag Nikolas Löbel CDU
Picha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

Nikolas Loebel  wa chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, na Georg Nuesslein kutoka chama kingine mshirika cha Christian Social Union, CSU wameamua kukaa pembeni baada ya kuwa katika mbinyo mkali kutoka kwa wenzao vyamani pamoja na wanasiasa wengine. Baada ya awali kusema angejiuzulu nafasi mamlaka yake ya kibunge mwishoni mwa Agosti, Loebel jana Jumatatu akatangaza moja kwa moja kujiondoa katika wadhfa huo.

Amesema anafanya uamuzi wa kujizulu kwa lengo la kuepusha kukiathiri chama chake zaidi. Na Nuesslein, ambaye alikuwa naibu kiongozi wa muungano wa kambi ya CDU-CSU katika bunge la Ujerumani hadi kujiuzulu kwake Ijumaa iliyopita, amesema atasalia kuwa mbunge hadi mwishoni mwa muhula wa bunge la sasa ambao ni Septemba.

Nuesslein ajiuzulu haraka katika nafasi ya ubunge

Markus Söder CSU Ministerpräsident Bayern
Kiongozi wa chama cha CSU Markus SoederPicha: SvenSimon/picture alliance

Lakini kiongozi wa chama cha CSU, Markus Soeder, amemtaka Nuesslein kufuata nyayo za Loebel kuondoka katika nafasi yake ya ubunge mara moja. Wanasiasa wote hao wawili wanakabiliwa na tuhuma za kujinufaisha kwa kusaidia mazungumzo yaliyofanikisha kandarasi ya manunuzi ya barakoa. Ijumaa iliyopita hata Loebel mwenyewe alithibitisha kuhusika wake katika biashara hiyo, ambayo kampuni yake iliweza kujipatia kiasi cha Euro 250,000.

Pamoja na kuwa kugoma kuondoka mara moja katika wadhfa wake, Nuesslein amekanusha tuhuma kwamba amefaidika na Euro 600,000, kwa kupitia kampuni ya kutoa ushauri ya ununuzi wa barakoa huko jimboni Bavaria.

Uwezekano wa kuandaliwa mashtaka ya rusha na hongo

Waendesha mashtaka mjini Munich wanachunguza uwezekano wa kumwandalia mashtaka Nuesslein ya kutoa hongo na rushwa.

Mada hiyo imezidi kushika kasi nchini Ujerumani, ikiwa inatokea siku chache kabla ya uchaguzi wa majimbo wa Baden-Wuerttenberg na Rhineland-Palatinate, ambao unatarajiwa kufanyika Jumapili. Kambi yao, au ushirika wa vyama ndugu vya CDU na CSU kwa pamoja upo katika harakati za kuhakikisha hakuna kinachoathiri matokeo ya uchaguzi huo kwa upande wao.

Lakini kiongozi mwenza wa chama cha watetezi wa mazingira The Greens, Robert Habeck ambao wametoa uchunguzi wa maoni wa kitaifa amesema kuna utata unaonesha kuna matatizo ya kimuundo na kimfumo katika muungano wa vyama vya CDU/CSU.

 

Chanzo: DPAE