1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGambia

Wabunge nchini Gambia waunga mkono ripoti dhidi ya ukeketaji

9 Julai 2024

Wabunge nchini Gambia wameidhinisha ripoti ya kamati inayounga mkono marufuku ya mwaka 2015 dhidi ya ukeketaji wanawake, wakati muswada unaotaka kubatilisha sheria hiyo unatarajiwa kupigiwa kura mwisho wa mwezi huu

https://p.dw.com/p/4i23S
Maandamano ya kupinga ukeketaji wanawake nchini Gambia mnamo Machi 18, 2024. Gambia huenda likawa taifa la kwanza duniani kubatilisha marufuku dhidi ya ukeketaji wanawake
Maandamano ya kupinga ukeketaji wanawake nchini GambiaPicha: Hadim Thomas-Safe Hands for Girls/AP/picture alliance

Kamati ya pamoja ya afya na jinsia iliwasilisha mrejesho wake Jumatatu ikisema marufuku ya mwaka 2015 dhidi ya ukeketaji wanawake inapaswa kudumishwa kuzuia tohara ya wanawake kwa aina zote nchini Gambia.

Ukeketaji unahatarisha maisha ya wanawake na wasichana

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuondoa marufuku ya ukeketaji wanawake kunawaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa za kiafya pamoja na kukiuka haki yao ya ustawi wa kimwili na kiakili.

Soma pia:HRW yawataka wabunge wa Gambia kutoruhusu ukeketaji

Kamati hiyo imesema imeshauriana na wasomi wa Kiislamu waliothibitsha kuwa tamaduni hiyo sio hitaji la Uislamu, hoja ambayo hutumiwa sana na wanaharakati wa ukeketaji.

Ripoti dhidi ya ukeketaji wanawake yaidhinishwa kwa wingi wa kura 

Baada ya mabishano makali ambayo wakati fulani yalizua kelele,  wabunge 35 walipiga kura kuidhinisha ripoti hiyo, huku 17 wakipiga kura ya kuipinga na wawili wakikosa kupiga kura.