1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabulgaria wapania kuimaliza enzi ya waziri mkuu Borisov

11 Julai 2021

Rushwa na ufisadi ni kadhia zilizowakasirisha wananchi wengi wanaotaka mabadiliko katika nchi hiyo masikini ya Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/3wKAZ
Bulgarien Wahl Parlamentswahl 2021
Picha: Spasiyana Sergieva/REUTERS

Wabulgaria wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi wa bunge utakaoamua ikiwa vyama vya upinzani vinaweza kuunda serikali mpya ijayo baada ya muongo wa siasa za nchi hiyo kuhodhiwa na waziri mkuu wa muda mrefu  Boyko Borisov.

Uchaguzi huu ni wa pili katika nchi hiyo ya Balkan katika kipindi cha miezi mitatu baada ya matokeo ya uchaguzi wa Aprili kushuhudia  bunge lenye mgawanyiko lililoshindwa kuunda serikali ,hali inayoonesha mgawanyiko mkubwa uliopo nchini Bulgaria kuhusu kile kinachoachwa na utawala wa waziri mkuu Borisov.

Chama chake cha GERB kinaonesha kukaribiana kabisa kwenye uchaguzi huo na chama kipya cha upinzani chenye msimamo mkali cha -Ima Takav Narod (ITN) kinachoongozwa na mtangazaji wa Televisheni Slavi Trifonov ambapo inaonesha kila upande unaelekea kupata kiasi asilimia 20 hadi 22 ya kura huku kura za maoni zikionesha chama hicho tawala kinaongoza kwa tafauti ndogo sana.

Bulgarien | Armut
Picha: Artur Widak/NurPhoto/picture alliance

Wachambuzi wanaeleza  kwamba hata ikiwa chama cha mrengo wa kulia cha siasa za wastani- GERB kitafanikiwa kuongoza kwenye uchaguzi huu wa bunge,Borisov mwenye umri wa miaka 62 aliyewahi kuwa mlinzi wa dikteta wa zamani mkomunisti  Todor Zhivkov hana uwezekano wa kupata washirika wa kuunda nae serikali ya mseto kufuatia hasira za wananchi kuhusiana na ufisadi uliozagaa nchini humo.

Mchambuzi wa kisiasa Parvan Simeonov kutoka shirika la kimataifa la Gallup lenye makao yake mjini Sofia anahisi kwamba huu utakuwa mwisho wa enzi ya Borissov.Mchambuzi huyo anasema watu wa Bulgaria wamechochswa na mtindo wake wa uongozi kwa ujumla  na zaidi ya yote wamechoshwa na tuhuma za rushwa zilizoko nchini humo.Uungaji mkono wa chama cha ITN na vyama vingine viwili vidogo vinavyopinga rushwa vya Democratic Bulgaria na Stand Up!Mafia Out! umeongezeka tangu uchaguzi wa Aprili.

Bulgarien Wahl Parlamentswahl 2021 Hristo Ivanov
Picha: Hristo Rusev/Getty Images

Hata hivyo ITN na vyama vyenye uwezekano wa kuwa washirika wake huenda wakapata taabu  kuunda serikali bila ya kuungwa mkono na baadhi ya vyama vikubwa vilivyozoeleka nchini humo.

Nikolay Galabov mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni mhandisi, baada ya kupiga kura yake alisema kwamba  vijana wenye umri mdogo wanaendele kuikimbia nchi kuelekea nje na ufisadi unakandamiza juhudi zozote za kibiashara na kwahivyo anaamini ni lazima yafanyike mabadiliko.

Vyama vya upinzani vilivyokuwa vikiunga mkono maandamano nchini humo,ambavyo vinataka kuimarisha uhusiano na washirika wa Bulgaria katika jumuiya ya kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya vimeahidi kuitia nguvu idara ya mahakama ili kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za msaada zinazotarajiwa kumiminika nchini humo kama sehemu ya

fungu la kuisaidia nchi hiyo kujikwamua kutokana na janga la virusi vya Corona.

Bulgarien | Smog in Sofia
Picha: Hristo Rusev/Getty Images

Bulgaria nchi masikini kabisa katika Umoja wa Ulaya imekuwa na historia ya muda mrefu ya rushwa na ufisadi lakini kadhia kadhaa za hivi karibuni pamoja na hatua ya Marekani ya  kuwawekea vikwazo mwezi uliopita raia wengi wa Bulgaria kutokana na madai ya kuhusika na ufisadi ni suala lililohodhi kwa sehemu kubwa kampeini ya uchaguzi.

Serikali ya mpito iliyoko sasa imelituhumu baraza la mawaziri la waziri mkuu Borissov kwa kutumia mabilioni ya fedha za walipa kodi bila ya kuzingatia utaratibu wa wazi  miongoni mwa makosa mengine .Lakini chama cha GERB cha waziri mkuu huyo kimekanusha kufanya makosa yoyote na kusema madai yanayotolewa yamechochewa kisiasa. Ikumbukwe kwamba baraza la mawaziri la  sasa la mpito liliteuliwa na rais Rumen Radev ambaye ni mkosoaji mkubwa wa waziri mkuu Borissov,baraza hilo liliundwa baada ya uchaguzi wa Aprili kushindwa kumpaka mshindi.

Borissov mwenyewe anasema waziri wa mambo ya ndani  anaendesha ukandamizaji kama uliofanyika enzi za Ukomunisti  dhidi ya chama cha GERB kwa lengo la kuwafaidisha  wapinzani wake  na kwamba uchaguzi huu wa Jumapili tayari matokeo yamesha chakachukuliwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Tatu Karema

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW