Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wadai kuuteka mji wa Goma
27 Januari 2025M23 wametangaza kuukamata mji huo katika taarifa, dakika chache kabla ya kumalizika muda wa masaa 48 uliowekwa na kundi hilo kwa jeshi la Kongo kusalimisha silaha zao. Waasi hao wamewahimiza raia wa Goma kuwa watulivu na kwa wanajeshi wa Kongo kukusanyika katika uwanja mkuu wa michezo. Shirika la Human Rights Watch limesema mzozo wa mashariki ya Kongo unaweza kuwa janga la kibinadamu.
Jumapili usiku, walinda amani wa Umoja wa Mataifa walianza kuwasajili askari waliojisalimisha viungani mwa mji wa Goma. Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya ametoa wito wa ulinzi wa raia akisema nchi iko katika hali ya vita ambapo habari zinabadilika kila wakati.
Huku wakisaidiwa na maelfu kadhaa ya askari wa Rwanda, waasi wa M23 katika siku za karibuni wamesonga mbele kwa kasi wakikabiliana na wanajeshi wa Kongo wanaoulinda mji huo.
Wanajeshi kadhaa wa kigeni wa kulinda amani wameuawa katika makabiliano hayo, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka Kigali kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo – wito uliokataliwa na Rwanda.
Katika taarifa Jumapili, wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilisema inalazimika kuchukua hatua ya kuendelea kujihami na kujilinda kwa sababu ya mapigano yanayoendelea karibu na mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Lakini Rais wa Kenya William Ruto Jumapili usiku alitangaza mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na viongozi wa Rwanda na DR Kongo kuujadili mzozo huo. Taarifa ya Ruto ilisema Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda wamekubali kuhudhuria mkutano huo wa kilele katika siku mbili zijazo.
Kwenye kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa mambo ya nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner alisema Rwanda inafanya "uchokozi wa wazi, tangazo la vita ambalo halijifichi tena nyuma ya ujanja wa kidiplomasia." Vyanzo vya Umoja wa Mataifa viliiambia AFP kati ya askari 500 na 1,000 wa Rwanda waliwasili Jumapili kujiunga na M23 karibu na Goma. Kayikwamba Wagner amelitaka baraza la usalama kuwawekea maafisa wa Rwanda vikwazo.
Naye balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa Ernest Rwamucyo, hakuthibitisha au kukanusha madai hayo. Ameilaumu serikali ya Kongo, akisema mzozo huo ungeweza kuepukika kama "ingeonyesha dhamira ya kweli ya amani."
Kongo na Rwanda zimewaita nyumbani mabalozi wao na kuvunja mahusiano ya kidiplomasia.
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo aliuambia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kutokana na uwanja wa ndege kufungwa na barabara kufungwa katika kitovu hicho kikubwa cha misaada ya kibinadamu na usalama katika eneo hilo, "tumenaswa."
Bintou Keita, aliuambia mkutano huo kuwa licha ya msaada wa askari wa kulinda amani kwa jeshi la Kongo, waasi wa M23 na askari wa Rwanda waliingia kitongoji cha Munigi, viungani mwa Goma, na kusababisha hofu kubwa. Keita alisema wapiganaji wa M23 walikuwa wakisonga mbele kwa kuwatumia wakazi "kama ngao ya binadamu” huku wengine wakikimbilia usalama wao.
Baraza la Usalama limelaani kupuuzwa kwa waziwazi kwa uhuru na uadilifu wa mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Limewataka wanajeshi wa nje waondoke, bila kuwataja moja kwa moja.
Awali, mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres alirudia kulaani vikali mashambulizi ya M23 kwa msaada wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda," na kutoa wito kwa kundi hilo la waasi kusitisha mara moja vitendo vyote vya uhasama na kujiondoa, alisema msemaji Stephane Dujarric.
afp, ap, reuters, dpa