1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Tigray wapuuza usitishaji wa vita wa Ethiopia

Daniel Gakuba
29 Juni 2021

Viongozi TPLF katika jimbo la Tigray wamepuuza tangazo la kusitisha vita lililotolewa na serikali kuu mjini Addis Ababa jana, na wameapa kuendeleza mapambano hadi pale watakawafurusha kikamilifu wanajeshi wa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/3vkJS
Äthiopien I Konfliktregion Tigray
Wanajeshi wa Ethiopia wakipiga doria katika mji wa Mekele (07.03.2021)Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Tangazo hilo la TPLF la kukaidi hatua ya serikali ya kusitisha mapigano limekuja usiku wa kuamkia leo, muda mfupi baada ya wapiganaji wa chama hicho kusema wamechukua udhibiti wa mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele. Kabla ya hapo, serikali ya shirikisho la Ethiopia inayoongozwa na waziri mkuu Abiy Ahmed ilikuwa imechukuwa maamuzi ya upande mmoja ya kusitisha mapigano.

Soma zaidi: Ethiopia: Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele washambuliwa vikali

Katika tangazo hilo la TPLF, chama hicho ambacho kinachukuliwa na serikali kuu kama cha uasi kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha ukombozi na usalama wa watu wa jimbo la Tigray.  Getachew Reda, msemaji wa chama hicho, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa lengo la adui wanayepigana naye ni kulibana jimbo la Tigray na kuhakikisha kuwa watu wake wanasalimu amri, na kuapa kuwa hilo halitowezekana.

Äthiopien l Premierminister Ahmed Abiy
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Hamasa miongoni mwa wapiganaji wa TPLF

Katika mazingira hayo ya mafanikio, mmoja wa wapiganaji wa tawi la kijeshi la TPLF, Teheras Tsega Berhan amesema wapiganaji wao wana ari kubwa ya mapambano.

''Vijana wamejawa na hamasa na wanamiminika katika vituo vya mafunzo, kujiunga na mapambano. Adui yetu anazidi kudhoofika, na anashindwa,'' amesema Berhan.

Vita vya Tigray vimekuwa vikiendelea kwa karibu miezi minane, na kwa muda mrefu wapiganaji wa TPLF na viongozi wao walikuwa wanajichimbia vichakani bila kupiga hatua yoyote kubwa.

Soma zaidi: Waethiopia washiriki uchaguzi ambao ni mtihani kwa Abiy Ahmed

Lakini wiki iliyopita walianzisha mashambulizi makali wakati serikali ya Addis Ababa ikifanya uchaguzi katika majimbo mengine isipokuwa Tigray.

Äthiopien I Konfliktregion Tigray
Vita vya jimboni Tigray vimesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamuPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Addis Ababa yasisitiza 'inapambana na wahalifu'

Matokeo ya uchaguzi  huo bado hayajatangazwa lakini yanatarajiwa kumpa ushindi waziri mkuu Abiy na vyama vinavyomuunga mkono.

Msemaji wa TPLF anadai kuwa kabla ya muda mrefu watakuwa wamemaliza kazi ya kulifurusha jeshi la Ethiopia kutoka jimboni mwao, ili wakaazi wa jimbo hilo waweze kufanya kazi zao kama kawaida.

Soma zaidi: Ethiopia: Amnesty yadai 'mauaji ya wengi' yamefanyika Tigray

Serikali kuu ya mjini Addis Ababa haijatoa tamko kuhusu taarifa ya TPLF kuukamata mji wa Makele, na msemaji wake Dina Mufti hata anakanusha kuwepo kwa vita, akisema kinachoendelea ni kupambana na wahalifu.

''Hatusemi kuna vita, tunasema kuna operesheni ya kuhakikisha sheria inaheshimiwa. Mtu anapokiuka sheria ya nchi lazima awajibishwe.''

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amezungumza na pande mbili katika vita hivyo, na kuzikumbusha kuwa hali iliyopo ni ushahidi mwingine kuwa mizozo haisuluhishwi kwa mtutu wa bunduki.

 

afpe, ape