1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Houthi waelekea Oman kwa matibabu

3 Desemba 2018

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umesema waasi 50 wa Houthi wamesafirishwa kuelekea Oman kwa ajili ya matibabu huku Martin Griffiths akiwasili mjini Sanaa kwa mazungumzo na waasi.

https://p.dw.com/p/39MCp
Jemen Konflikt - UN-Flugzeug - Hilfe
Picha: picture alliance / dpa

Kuondolewa waasi hao mjini Sanaa kupitia ndege ndogo ya Umoja wa Mataifa kunafungua njia ya majadiliano yaliyokwama ya kutafuta amani nchini Yemen huku viongozi wa dunia wakishinikiza kumalizika mapigano yaliyodumu miaka minne yalioisukuma Yemen katika hatari ya kukabiliwa na njaa.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Yemen Martin GriffithsPicha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, amesema ndege hiyo itawabeba waasi hao 50 pamoja na madaktari watatu wa Yemen kutoka Sanaa hadi katika mji mkuu wa Oman, Muscat. Hatma ya waasi walioumia lilikuwa moja ya mambo yaliokwamisha kuanza kwa mazungumzo ya amani yaliyofeli mwezi Septemba.

Umoja wa Mataifa unajaribu kuwaweka pamoja waasi wa Houthi nan a serikali inayoungwa mkono  na Saudi Arabia kukaachini katika meza ya mazungumzo mwezi huu. 

Huku hayo yakiarifiwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Yemen Martin Griffiths amewasili mjini Sanaa hii leo, kwa mazungumzo na waasi kuelekea jaribio jingine la mazungumzo ya amani kuleta pande zinazohasimiana katika meza ya mazungumzo.

Ziara yake inakuja wakati kukiwa na shinikizo la kufungua uwanja wa ndege unaoshikiliwa na waasi iliofungwa kwa zaidi ya miaka mitatu kufuatia mashambulizi ya angani yaliofanywa na muungano wa Saudi Arabia. Umoja wa Mataifa umesema kufunguliwa kwa uwanja wa ndege huo  ni kipaumbele katika azungumzo ya kurejesha amani ya Yemen.

Iran yaunga mkono juhudi za kurejesha amani Yemen

Wakati huo huo Iran imeunga mkono juhudi za mazungumzo yamani zinazofanywa na Umoja wa Mataifa ikitoa wito wa kumalizika kwa mateso nchini Yemen.

Iran Parlamentssitzung Abstimmung zum Anti-Terror-Gesetz
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Javad Zarif, Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi

Katika taarifa yake waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Javad Zarif, amesema wapenda vita bado hawajapata mafanikio yoyote ya kisiasa katika miaka minne ya mapigano na uchokozi uliofanywa kwa watu wa Yemen.

Wizara ya kigeni imesema viongozi wa dunia wanapaswa kushinikiza wasafirishaji wa silaha kwa makundi ya kihalifu kuunga mkono mazungumzo ya amani na kuwawachia wayemeni wenyewe kuamua mambo yao bila ya kuingiliwa na mataifa ya nje.

Mataifa ya Guba ya kiarabu pamoja na Marekani zinaishutumu Iran kwa kuwaungamkono waasi wa Houthi na kuliona hili kama kisingizio cha kuendelea na kampeni yake ya kijeshi ilioanzisha kuanzia mwezi Machi mwaka 2015.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef