Waandishi wa habari Afrika waaswa kuwasaidia wananchi
2 Mei 2022Wito huo umetolewa na waziri wa habari wa Tanzania Nape Nauye, katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yanayofikia kilele chake siku ya Jumanne.
Katika maadhimisho haya yanayozihusisha nchi takribani 10 za bara la Afrika, waziri wa habari wa Tanzania Nape Nauye , pamoja na mambo mengine amewaambia waandishi wa habari kwamba wanalo jukumu kubwa la kutumia taaluma zao na kuhahakikisha wanaisaidia Afrika kunufaika na rasilimali zake kama vile madini, ardhi, mito maziwa na bahari, akisema Afrika ni Tajiri na haipaswi kuendelea kuwa kama ilivyo sasa.
Akizungumzia upande wa majukumu ya serikali ya Tanznaia katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza waziri Nape amebainisha kuwa, kwa sasa kuna mabadiliko makubwa yanayofanyika kupitia wizara yake ya habari akitaja mchakato wa marekebisho ya sheria ya huduma za habari ya Tanzania ya mwaka 2016, pamoja na kanuni zake za mwaka 2017, kama mfano wa kushughulikia matatizo yanayoikumba sekta ya habari nchini Tanzania.
Katika mawasilisho ya mada mbali mbali za washiriki kutoka nchini nyingine barani Afrika, imeonekana kwamba kumekuwa na matatizo makubwa ya uhuru wa habari kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ikiwepo, wamiliki wa vyombo vya habari mitandaoni kulazimishwa kuondoa maudhui yao mitandaoni, mashambulizi ya kimtandao katika baadhi ya nchi, pamoja na kuminywa kwa uhuru wa watu kutoa maoni au kujieleza hasa katika kipindi cha uchaguzi. Nje ya ukumbi wa mikutano, katibu mkuu wa baraza la habari Tanzania Kajubi Mkajanga,pamoja na kusifu juhudi za serikali ya Tanzania kwa sasa za kuonesha mwanya wa kuwepo kwa uhuru wa kujieleza lakini anakosoa baadhi ya mambo. Waandishi wa habari mjini Bukavu waandamana kupinga ukatili dhidi yao
Miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika maadhimisho haya, ni pamoja na uandishi wa habari na changamoto za kidijitali, matumizi ya teknolojia katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kujenga mshikamano wa waandishi wa habari wa bara la Afrika. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni uandishi wa habari na changamoto za kidijitali.