1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wayavamia makao ya Rais Sri Lanka

9 Julai 2022

Rais Gotabaya Rajapaksa anaripotiwa kuhamishwa na kupelekwa mahali salama baada ya makundi ya watu kuvunja kizuizi kilichokuwa kimewekwa na maafisa wa polisi.

https://p.dw.com/p/4Dtj1
Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Picha: AFP/Getty Images

Sri Lanka inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi tangu ipate uhuru huku kukiwa na uhaba mkubwa wa mafuta na madawa.

Makumi kwa maelfu ya waandamanaji wanaomtaka Rais Rajapaksa na serikali yake wajiuzulu wamevamia makaazi yake rasmi Jumamosi. Rajapaksa amepelekwa mahali salama, amesema afisa mmoja katika afisi yake alipokuwa akizungumza na shirika la habari la dpa naye afisa mmoja mwandamizi wa ulinzi amesema "rais amesindikizwa na kupelekwa mahali salama."

Wakati wa maandamano hayo katika makao ya Rajapaksa, jambo ambalo limekuwa likifanyika mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni, maafisa wa usalama wamefyatua risasi hewani ili kujaribu kuwazuia waandamanaji kuwazidi nguvu na kuliteka kasri la rais, ila mwishowe waandamanaji hao walifanikiwa kuwazidi nguvu.

Waziri Mkuu aita mkutano wa dharura wa wakuu wa vyama

Kutokana na swintofahamu hiyo ya Jumamosi, Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe ameita mkutano wa dharura wa wakuu wa vyama vya kisiasa.

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung im Präsidentenpalast
Waandamanaji wakiwa ndani ya kasri la raisPicha: News Cutter/REUTERS

Ametoa wito kwa spika pia kuita kikao cha bunge cha dharura, imesema taarifa kutoka afisi ya waziri mkuu.

Wickremesinghe awali aliwahi kueleza nia yake ya kutaka kuunda serikali ya kitaifa kwa kuvishirikisha vyama vyote vya kisiasa.

Kisiwa cha Sri Lanka kinakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi tangu kilipopata uhuru mwaka 1948.

Rais amekataa kujiuzulu hadi sasa ila katika hatua ya kutaka kuwaridhisha waandamanaji, amewaachisha kazi jamaa zake kadhaa waliokuwa wanashikilia nyadhfa za juu serikalini, wakiwemo ndugu zake wawili waliokuwa wanahudumu kama waziri mkuu na waziri wa fedha.

Mnamo Mwezi Mei, Wickremesinghe aliteuliwa kama waziri mkuu na kwa sasa yeye ndiye anayeiongoza wizara ya fedha. Ameahidi kuanzisha mpango wa kuwaletea unafuu wa maisha raia na mpango mpya wa kiuchumi, ambao utamkubalia aitishe msaada wa kifedha wa kuiokomboa nchi hiyo kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani IMF.

Sri Lanka | Proteste gegen die Regierung
Polisi wakitumia maji na mabomu ya ktuoa machozi kuwatawanya waandamanajiPicha: Dinuka Liyanawatte/REUTERS

Nchi muflisi iliyo na madeni ya zaidi ya dola bilioni 50

Wickremesinghe amesema mazungumzo ya kuikomboa nchi hiyo kifedha na IMF yalikuwa yanategemea kumalizika kwa mpango wa kulilipa deni la nchi ifikiapo mwezi Agosti, na hichi kimekuwa kizingiti kwa nchi imefilisika, huku madeni sasa yakifikia dola bilioni 50.

Watu milioni 22 raia wa Sri Lanka wamekabiliwa na mfumko wa bei unaozidi kwa miezi kadhaa pamoja na muda mrefu wa kukosekana kwa nguvu za umeme baada ya serikali kukosa fedha za kigeni za kununua bidhaa kama chakula, mafuta na madawa.

Chanzo: AP/DW