1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Sudan watangaza uasi wa kiraia nchi nzima

Sylvia Mwehozi
9 Juni 2019

Upinzani nchini Sudan umetangaza kufanya kampeni ya uasi wa kiraia wa nchi nzima kuanzia Jumapili (09.06.2019) hadi pale baraza la kijeshi la mpito litakapokabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3K5Zo
BG Sudan Proteste
Picha: picture-alliance/dpa/AP

Tangazo hilo lililotolewa na chama cha wanataaluma wa Sudan SPA, ambacho awali kilianzisha maandamano dhidi ya kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir aliyeondolewa madarakani, linakuja siku chache baada ya jeshi kuwashambulia waandamanaji na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha mjini Khartoum na hivyo kuvunja matumaini ya makabidhiano ya kidemokasia ya madaraka.

"Vuguvugu la uasi wa kiraia litaanza Jumapili na kukoma tu pale serikali ya kiraia itakapojitangaza yenyewe kupitia televisheni ya taifa", ilisema sehemu ya taarifa ya chama cha wanataaluma wa Sudan SPA. Tamko lao linakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kukutana kwa nyakati tofauti na majenerali wanaotawala na viongozi wa waandamanaji katika juhudi za kufufua mazungumzo ambayo yalikaribia kuvunjika baada ya waandamanaji waliopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi kutawanywa siku ya Jumatatu.

Kamati kuu ya chama cha Madaktari wa Sudan, ambao ni moja ya makundi ya waandamanaji imesema kiasi cha watu 113 waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa tangu siku ya Jumatatu. Inasema takribani miili 40 imeopolewa kutoka mto Nile mjini Khartoum na kuchukuliwa na vikosi vya usalama tangu kuzuka kwa ghasia. Chama cha wanataaluma wa Sudan ambacho kiliongoza maandamano yaliyomuondoa Bashir, kimesema kinakubaliana na usuluhishi wa waziri mkuu Ahmed lakini kikatoa masharti kabla ya kurejea meza ya mazungumzo.

Sudan Krise Vermittlungsversuch Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akizungumza na muungano wa mabadiliko na uhuru. Picha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Masharti ya waandamanaji

Miongoni mwa masharti hayo ni kuanzishwa kwa tume huru itakayoungwa mkono kimataifa kwa ajili ya kuchunguza vurugu zote zilizojitokeza baada ya Al-Bashir kuondolewa mamlakani na kisha kuwachukulia hatua waliohusika. Chama hicho pia kinataka kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa na kwamba mazungumzo ya upatanishi yajikite zaidi katika makabidhiano ya madaraka kwa serikali ya kiraia.

Msemaji wake Mohammed Yousef al-Mustafa amedai kuwa juhudi za waziri mkuu wa Ethiopia zilituama zaidi katika kurejesha makubaliano ya awali baina ya Baraza la Kijeshi na muungano wa uhuru na mabadiliko unaowawakilisha waandamanaji. Kiongozi wa baraza la kijeshi Jenerali Abdel-Fattah Burhan alisema mapema wiki hii kwamba makubaliano yote ya awali yasingetiliwa mkazo.

Al-Mustafa amesema waziri mkuu Ahmed amependekeza baraza litakalokuwa na nafasi nane kwa ajili ya raia, na saba kwa ajili ya jeshi huku uongozi ukiwa ni wa kupokezana. "Tunakubaliana na pendekezo la waziri mkuu wa Ethiopia. Lakini hatutoketi meza moja na baraza la kijeshi hadi pale matakwa yetu yatakapotimizwa", alilieleza shirika la habari la Associated Press.

Nalo baraza la kijeshi katika taarifa yake fupi siku ya Jumamosi limeukubali mpango huo wa Ahmed na kurejelea wito wake wa kuanzisha tena mazungumzo "katika mazingira ya kuridhisha".

Ethiopian Prime Minister Abiy Ahmed
Viongozi wa upinzani Sudan waliokutana na waziri mkuu Ahmed katika ubalozi wa Ethiopia mjini Khartoum Picha: Reuters/M.N. Abdallah

Viongozi wa upinzani wakamatwa

Wakati huo huo vikosi vya usalama vimewakamata viongozi muhimu wa upinzani. Miongoni mwao ni Mohammed Esmat ambaye alikuwa mpatanishi wa waandamanaji na alikamatwa baada ya kukutana na waziri mkuu Abiy Ahmed siku ya Ijumaa mjini Khartoum. Pia vikosi vya usalama vilimkamata Ismail Jalab ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la ukombozi wa watu wa Sudan-kaskazini sambamba na msemaji wake Mubarak Ardol mapema siku ya Jumamosi.

Balozi wa Uingereza mjini Khartoum Irfan Siddiq amelaani kukamatwa kwa viongozi hao na kutoa wito kwa baraza la kijeshi kuwaachilia. Hapakuwa na kauli kutoka kwa Baraza la kijeshi juu ya kukamatwa kwa viongozi hao wa upinzani.

AP/AFP/Reuters