1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Sudan wadai utawala wa kiraia haraka

Sekione Kitojo
14 Aprili 2019

Watayarishaji wa maandamano nchini Sudan ambayo yamelazimisha kiongozi wa muda  mrefu al-Bashir kuondolewa madarakani  wanalitaja jeshi kukabidhi madaraka, "mara moja na bila masharti" kwa serikali ya mpito ya kiraia 

https://p.dw.com/p/3Gka9
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Picha: picture-alliance/AA

Waandamanaji  wamedai  kuundwa  serikali ya  kiraia haraka iwezekanavyo na  bila  masharti  ambayo  itatawala kwa  muda  wa  miaka  minne.

Vyama  vya  kisiasa  na  vuguvugu  lililokuwa  nyuma  ya  miezi minne  ya  maandamano  vimesema  katika  taarifa  ya  pamoja  jana Jumamosi (13.04.2019) kwamba watabaki  mitaani  hadi  pale  madai yao  yatakapofikiwa. Wamesema  hatua ya  kukabidhi  madaraka katika  serikali  ya  kiraia itakuwa  hatua  ya  kwanza  kuelekea katika  kuanguka  kwa  utawala.

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji mjini Khartoum wakiendelea na maandamano, wanadai jeshi likabidhi madarakaPicha: Getty Images/AFP/M. Hemmeaida

Jeshi  limeteua  baraza  la  kijeshi  ambalo inasema  litatawala  kwa miaka  miwili  ama pungufu  wakati  uchaguzi  ukitayarishwa.  Baraza hilo  lilikutana  na  ujumbe  wa  watayarishaji  wa  maandamano  jana Jumamosi.

Jeshi lilimpindua  al-Bashir siku  ya  Alhamis, na  kufikisha  mwisho karibu  miaka  30 ya  utawala  wake  na  kumuweka  chini  ya kizuwizi cha  nyumbani kwake  katika  mji  mkuu  Khartoum. Waandamanaji wanahofu kwamba  jeshi , ambalo linadhibitiwa na  wateule  wa  al-Bashir, litang'angania  madarakani ama  kumchagua  mmoja  kati yao  kumrithi.

Saudi Arabia  na  Umoja  wa  falme za  Kiarabu wakati  huo  huo zimetoa  taarifa  kuunga  mkono  baraza  la  keshi  la  mpito  nchini. saudi Arabia  imesema "inasimama pamoja  na  watu  wa  Sudan"  na kutoa  wito kwa  wasudan wote "kutoa umuhimu kwa  maslahi  ya kitaifa"  kwa  nchi  yao.

Umoja  wa  Falme  za  Kiarabu UEA , imewataka wasudan "kufanyakazi kwa  ajili  ya  kulinda uhalali  na  kuhakikisha  mabadiliko ya  amani  ya  madaraka."

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji mjini KhartoumPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mfalme  wa  saudia  Salman  ameamuru  kiasi  ambacho  hakikutajwa cha  misaada  kwa  Sudan  ambayo  ni  pamoja  na  bidhaa za mafuta  ya  petroli , ngano  na  madawa.

Katika  taarifa  nyingine  tofauti  iliyotolewa  jioni  ya  jana Jumamosi, Saudi Arabia  na  UAE hususan zilielezea uungaji  wao mkono  wa  baraza la  mpito  la  Sudan  lililoundwa  na  jeshi.

Amri ya hali ya hatari

UAE imesema inakaribisha  kuapishwa  kwa  jenerali Abdel - Fattah Burhan siku  ya  Ijumaa  kuwa  mkuu  wa  baraza  hilo.

Burhan  amechukua uongozi  wa  baraza  la  kijeshi  siku moja  baada ya  kuondolewa  kwa  al-Bashir baada  ya  waandamanaji  kupinga baraza  hilo  kuongozwa  na  jenerali Awad ibn Ouf, ambaye anaonekana  kuwa  yuko  karibu  sana  na  al-Bashir.

Katika  matamshi  yaliyotangazwa  katika  televisheni  ya  taifa , Burhan  alisema  Jumamosi  baraza  limewaalika "makundi  yote  ya Wasudan  katika majadiliano."

Sudan | Awad Ibn Auf als Präsident des militärischen Übergangsrates vereidigt
Awad Ibn Auf waziri wa ulinzi wa Sudan akiapishwa kuwa mkuu wa baraza la kijeshi la Sudan. Waandamanaji wamemkataa.Picha: picture-alliance/AA

Amesema  anaondoa amri  ya  kutotembea  usiku iliyowekwa  siku ya  Alhamis, ambayo  ilikuwa  idumu  kwa  muda  wa  mwezi  mmoja, na  kutangaza  kuachiwa  mara  moja kwa  wale  waliokamatwa  na kuwekwa  kizuwizini  na  kufikishwa  mahakamani  chini  ya  wimbi  la machafuko  ambayo  yalianza  Desemba  mwaka  jana.

Al-Bashir  aliweka  amri  ya  hali  ya  hatari  mwezi  Februari, akipiga marufuku mikusanyiko ambayo haikuidhinishwa  na  kutoa  madaraka makubwa  kwa  polisi  katika  juhudi  za kuzima maandamano. Dazeni kadha  za  watu waliuwawa  katika  mapambano kati ya polisi  na waandamanaji, na  mamia  wamehukumiwa  katika  mahakama  za dharura.

Demonstration Sudan Karthoum
Waandaamnaji wakiwa katika makao makuu ya jeshi mjini KhartoumPicha: Reuters

Waandamanaji  wamelielekeza vuguvugu  lao  katika  mapinduzi  ya umma  ya  mataifa  ya  Kiarabu  ya mwaka  2011 ambayo yamewaondoa  viongozi  kutoka  madarakani nchini  Misri, Tunisia, Libya na  Yemen. Wamechukua  nyingi  ya  nyimbo  na kauli  mbiu, na  kuchukua  hatua  za  kukaa  nje  ya  makao  makuu  ya  jeshi mjini  Khartoum mapema mwezi huu.

Mapinduzi  ya  aina  hiyo yameacha  mchanganyiko wa  hali halisi, ambapo  ni  Tunisia  pekee iliyojitokeza kuwa  na utawala  wa kidemokrasia.