1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vurugu zazuka, polisi wa Israel waingia msikiti wa Al-Aqsa

5 Aprili 2023

Polisi ya Israeli imewakamata zaidi ya watu 350, baada ya makabiliano kuzuka katika msikiti wa Al-Aqsa mapema Jumatano.

https://p.dw.com/p/4PiVM
Maafisa wa polisi wa Israel wamkamata Mpalestina mmoja wakati vurugu zilipozuka katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa Jerusalem Aprili 5, 2023.
Maafisa wa polisi wa Israel wamkamata Mpalestina mmoja wakati vurugu zilipozuka katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa Jerusalem Aprili 5, 2023.Picha: AHMAD GHARABLI/AFP/Getty Images

Hayo yamejiri wakati maafisa wa polisi walipoingia kwenye msikiti huo kuwatimua wale waliowaita kuwa wachochezi. Hatua hiyo imeshutumiwa vikali na Hamas ambalo ni Vuguvugu la Kiislamu la Palestina. 

Wanamgambo wa Palestina walijibu uvamizi wa polisi wa Israel kwa kufyatua roketi kuelekea Israel kutoka ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas.

Hatua iliyosababisha Israel kujibu kwa mashambulizi ya angani.

Machafuko hayo yamejiri wakati kuna mvutano mkubwa Jerusalem mashariki na pia wakati mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa waumini wa Kiislamu, ukiambatana na likizo ya Pasaka ya Wayahudi.

Vuguvugu la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza, limewataka Wapalestina walioko ukingo wa Magharibi kuenda kwa wingi katika msikiti wa Al-Aqsa kwa kile walichosema ni kuulinda msikiti huo.

Polisi ya Israel imesema maafisa wake waliingia ndani ya msikiti huo kuwaondoa wale waliowataja kuwa wachochezi, waliojifungia humo ndani kwa fataki, fimbo na mawe. Polisi imeongeza kuwa waliwakamata zaidi ya watu 350.

Polisi wa Israel wakishika doria katika eneo la Msikiti Al-Aqsa mjini Jerusalem huku mwanamke Mpalestina akiketi karibu na maafisa hao wa mpakani.
Polisi wa Israel wakishika doria katika eneo la Msikiti Al-Aqsa mjini Jerusalem huku mwanamke Mpalestina akiketi karibu na maafisa hao wa mpakani. Picha: Ammar Awad/REUTERS

Eneo tete la msikiti wa Al-Aqsa

Kwa muda mrefu, msikiti wa Al-Aqsa ulioko mashariki mwa mji mkongwe wa Jerusalem, umekuwa kitovu cha mvutano kati ya Wapalestina na vikosi vya usalama vya Israel. Mvutano huo hutokea hususan katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambapo maelfu kwa maelfu ya waumini wa Kiislamu hushiriki ibada.

Msikiti huo ambao ni eneo la tatu takatifu zaidi kwa Waislamu, umejengwa katika kile Wayahudi hukiita Mlima wa Hekalu, ambalo ni eneo takatifu zaidi la Wayahudi.

Mvutano mkali waibuka Umoja wa Mataifa juu ya ziara ya Al-Aqsa

Machafuko hayo mapya yamejiri  katika nusu ya kipindi cha Ramadhan na wakati Wayahudi wanajiandaa kusherehekea Pasaka kuanzia Jumatano usiku.

Polisi ya Israel ilitoa kanda ya video iliyoonesha kile kilichoonekana na milipuko ya fashifashi ndani ya msikiti huo na watu wakirusha mawe.

Kanda za video za polisi

Kanda nyingine ya video ya polisi inaonesha polisi wa kupambana na vurugu waliobeba ngao wakiingia msikitini huku kukiwa ni miripuko mingi.

Palestina yalaani ziara ya waziri wa Israel eneo la Al-Aqsa

Baadaye, kanda hiyo inaonesha mlango uliozibwa na vijisanduku vya miripuko sakafuni, huku polisi wakiwasindikiza nje watu wasiopungua watano waliofungwa pingu mikononi.

Polisi ya Israel imesema ililazimika kuingia msikitini humo baada ya vijana kadhaa waliokuwa wakivunja sheria na waliojifunga barakoa usoni kujifungia ndani ya msikiti huo.

Sehemu ya machafuko yaliyozuka katika msikiti wa Al-Aqsa Aprili 5, 2023, baada ya polisi ya Israel kuingia msikitini humo kuwaondoa "wachochezi".
Sehemu ya machafuko yaliyozuka katika msikiti wa Al-Aqsa Aprili 5, 2023, baada ya polisi ya Israel kuingia msikitini humo kuwaondoa "wachochezi".Picha: MOHAMMED ABED/AFP

Taarifa rasmi ya polisi imesema "hawa wachochezi walijiimarisha humo, saa chache baada ya sala ya Taraweeh, ili kuvuruga utulivu wa umma na kuuchafua msikiti”.

Polisi ya Israel: Lengo lilikuwa kuwaondoa ili kuruhusu maombi ya alfajiri

Taarifa hiyo imeongeza kuwa "baada ya majaribio kadhaa ya mazungumzo kuwataka waondoke kushindwa, polisi walilazimika kuingia ili kuwatimua kwa lengo la kuruhusu maombi ya alfajiri na kuzuia machafuko.

Jeshi la Israel limesema kufuatia machafuko hayo, makombora yasiyopungua tisa yalifyatuliwa kutoka ukanda wa Gaza kuelekea Israel.

Kulingana na jeshi hilo, makombora matano yalizuiwa na mfumo wa ulinzi wa angani, lakini manne yalishambulia maeneo yasiyokaliwa na watu.

Kwa kujibu mashambulizi hayo, ndege za kivita za Israel zilishambulia vituo viwili vinavyoshukiwa kuwa Hamas hutumia kutengeneza silaha, katika eneo la kati la ukanda wa Gaza. Hayo ni kulingana na jeshi la Israel.

Chanzo: AFPE