1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Volodymyr Zelensky atoa wito wa ushindi zaidi dhidi ya Urusi

25 Februari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewahimiza wapiganaji wake kupigania ushindi zaidi wa kijeshi wakati taifa hilo linapoendelea kukabiliana na uvamizi kamili wa vikosi vya Urusi nchini humo

https://p.dw.com/p/4Ny0r
Ukraine Kiew | Wolodymyr Selenskyj, Präsident
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine sasa umedumu kwa muda wa mwaka mmoja. Zelensky amesema kuwa ikiwa watakuwa makini, ushindi bila shaka unawasubiri akiongeza kuwa watashinda kwasababu ukweli uko upande wao. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa msaada kamili wa kimataifa katika harakati za jeshi la Ukraine za kuvifirusha vikosi hivyo vya Urusi.

Zelensky aelezea kumbukumbu ya siku aliyoiita mbaya zaidi

Akitafakari kuhusu vita hivyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Zelensky aliyaita mauaji ya raia katika eneo la Bucha kuwa wakati mbaya zaidi, akisema ilikuwa siku mbaya zaidi. Alielezea kumbukumbu ya miili ya raia waliokufa iliopatikana katika kitongoji hicho cha Kiev, wengine wakiwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo yao. Rais huyo ametoa wito kwa Urusi kufunguliwa mashitaka kwa uhalifu wa kivita.

Zelensky asema ''siku ya ushindi '' inakuja

Zelensky aliwaambia wanahabari kwamba, siku njema katika vita hivyo bado ziko mbele na kuziita ''siku za ushindi.'' Akijibu swali kuhusu tukio lililomkatisha tamaa zaidi, alisema kuwa watu wengi waliondoka katika mji mkuu na nchi hiyo kwa ujumla bila ya kutoa pingamizi yoyote.

Ukraine Krieg mit Russland Grab von Mykhailo Matiouchenko in Bucha
Eneo la makaburi mjini Bucha nchini UkrainePicha: Raphael Lafargue/abaca/picture alliance

Mapema, Zelensky alitoa hotuba katika kanisa la Mtakatifu Sophia mjini Kiev ambapo aliwatunuku wanajeshi medali za huduma. Waliohudhuria walidumisha ukimya wa dakika moja kwa heshima ya wahanga wa vita hivyo nchini Ukraine. Haya ni kwa mujibu wa shirika la habari la dpa.

Vita nchini Ukraine havioneshi dalili ya kumalizika

Vita hivyo ambavyo watu wengi walifikiri vingemalizika siku kadhaa baada ya kuanza, havioneshi dalili ya kumalizika mwaka mmoja baadaye huku pande mbili katika mgogoro huo zikikataa maafikiano ya aina yoyote. Katika masaa ya alfajiri mnamo Februari 24 mwaka 2022, vikosi vya Urusi vilivamia ngome za Ukraine katika maeneo kadhaa ya mipaka. Tangu wakati huo, Urusi imeteka maeneo manne Mashariki na Kusini mwa Ukraine kwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa. Awali wakati wa uvamizi huo, vikosi vya Urusi pia vilikuwa vimesonga mbele kueleka Kiev lakini kwasasa vimeondoka kutoka maeneo karibu na mji huo mkuu. Mapigano sasa yamekithiri katika maeneo ya Mashariki na Kusini makali zaidi yakiwa katika maeneo ya mji wa Bakhmut.