1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Vita vya Urusi na Ukraine vyatimiza mwaka mmoja

24 Februari 2023

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema Ukraine haijashindwa na imepambana na vizingiti vingi na kwamba itashinda dhidi ya uvamizi wa vikosi vya Urusi.

https://p.dw.com/p/4NtmB
Ukraine | Selenskyj in Zaporizhzhia
Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/AFP

Akizungumza Alhamisi, siku moja kabla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, Zelensky amesema watawawajibisha wale wote ambao wamesababisha uovu huo katika ardhi yao.

Wakati huo huo, shirika la ushirikiano wa mahakama la Umoja wa Ulaya, Eurojust limeanzisha kituo kipya cha kusaidia kukusanya ushahidi wa uhalifu uliofanywa nchini Ukraine, kutokana na uvamizi wa Urusi.

Eurojust yenye makao yake mjini The Hague, imetoa tangazo hilo siku ya Alhamisi wakati ambapo jumuia ya kimataifa imekuwa ikitoa wito wa kuwawajibisha wanaohusika na uhalifu wa kivita nchini Ukraine na kufunguliwa mashtaka, baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Ujerumani yataka nchi nyingine ziisaidie Ukraine

Huku hayo yakijiri Ujerumani imesema tayari inaiunga mkono Ukraine na sasa nchi nyingine zinapaswa kufanya hivyo pia. Hayo yameelezwa Alhamisi na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Christian Lindner wakati wa mkutano wa mawaziri wa fedha wa kundi la nchi saba tajiri duniani, G7, ambao wanakutana mjini Bengaluru, India kujadiliana jinsi ya kuisaidia kifedha Ukraine.

Mkutano huo utahudhuriwa pia na Waziri wa Fedha wa Ukraine, Serhiy Marchenko pamoja na magavana wa mabenki kuu. Mawaziri hao wa G7 wameiomba Benki ya Dunia kuipatia Ukraine msaada mpya wa fedha ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi.

Österreich | OSCE Treffen Ukraine in Wien
Wajumbe wakiwasili katika mkutano wa OSCEPicha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Ama kwa upande mwingie, wabunge wa Urusi wamekosolewa vikali kutokana na nchi yao kuhusika na vita vya Ukraine. Hayo yamejiri Alhamisi katika mkutano wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE mjini Vienna. Spika wa bunge la OSCE, Margareta Cederfelt amesema baadhi ya wabunge wanasaidia kuunga mkono uhalifu wa kichokozi.

''Binafsi naweza kusema kwamba swali lililopo ni kwa nini bunge la Urusi limewataka baadhi ya wajumbe wake kushiriki katika vikao vya bunge kuhusu amani na usalama barani Ulaya. Ni dalili kwamba Warusi hawapengi mazungumzo na wanapendelezea zaidi kuongeza mivutano kwa maneno yasiyo na msingi na yenye kuumiza,'' alifafanua Cederfelt.

Ukraine yasusia mkutano wa OSCE

Wabunge wa Ukraine wamesusia mkutano huo wakipinga ushiriki wa wabunge wa Urusi, hatua iliyosababisha mbunge mmoja wa Slovakia kuwaita wabunge wa Urusi wahalifu wa kivita na kwamba ushiriki wao ni kashfa kwa waathirika wa ukatili wao. Wabunge wa Lithuania pia wameususia mkutano huo wakionesha mshikamano na Ukraine.

Shirika la OSCE lenye nchi wanachama 57 linalenga kuzuia mizozo na kuimarisha demokrasia. Ndiyo jukwaa pekee la kikanda la usalama ambapo wanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO kama vile Marekani mara kwa mara wanakutana na Urusi. Hata hivyo, hakuna maamuzi yanayotarajiwa kufikiwa katika mkutano huo wa siku mbili.

(AFP, AP, DPA)