Vita Kongo vyasababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi Burundi
20 Februari 2025Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linakadiria kuwa karibu watu 30,000 wamevuka kuingia Burundi, huku idadi ikiendelea kuongezeka kila siku. Serikali ya Burundi imethibitisha kuwa angalau wakimbizi 10,000 wameingia kupitia mpaka wa magharibi wakikimbia ghasia katika DRC mashariki.
Mgogoro huu unatokana na mashambulizi mapya ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wamechukua udhibiti wa miji mikuu kama Goma na Bukavu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa M23 inaendelea kusonga mbele kuelekea maeneo mengine muhimu, jambo ambalo linaongeza hofu ya mgogoro mkubwa wa kikanda. Bukavu, lenye wakazi wapatao milioni moja, liko kilomita 50 tu kutoka Burundi, hivyo kuwa eneo muhimu kwa watu waliopoteza makazi wakisaka hifadhi.
Soma pia: Kongo: Waasi wa M23 wazidi kusonga mbele Kivu Kusini
Bintou Keita, mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO), alielezea wasiwasi wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi ya M23 yanakaribia makutano ya mipaka ya DRC, Rwanda na Burundi.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Huang Xia alionya kuwa hatari ya mzozo mkubwa wa kikanda sasa ni halisi zaidi kuliko wakati wowote. Burundi tayari imetuma zaidi ya wanajeshi 10,000 tangu Oktoba 2023 kusaidia jeshi la Kongo kupambana na M23 na makundi mengine yenye silaha.
Hata hivyo, ripoti zinaashiria kuwa baadhi ya wanajeshi wa Burundi wanajiondoa "kimkakati," ingawa jeshi la Burundi linakanusha madai ya kurudi nyuma.
Wakimbizi waliokwama mpakani
Wakimbizi wanaowasili Burundi wanasimulia jinsi walivyokimbia ghasia kutoka maeneo ya vita. Kitenge, kijana wa miaka 25 aliyekuwa dereva wa bodaboda, alikimbia na familia yake kabla M23 hawajafika, akisema makundi yenye silaha yalikuwa yakifyatua risasi kiholela, na kuwalazimu kukimbia ili kuokoa maisha yao.
Mkimbizi mwingine, Amissi, mwalimu kutoka Kamanyola, aliripoti kuwa maafisa wa Burundi waliwafungia kwenye uwanja wa michezo karibu na mpaka bila kuruhusu kwenda kununua chakula au bidhaa nyinginezo.
Soma pia: Vyanzo: Waasi wa M23 wameingia mji wa Bukavu
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, Martin Niteretse, alisema kuwa serikali inapanga kuwahamishia wakimbizi mashariki mwa Burundi ili kuhakikisha usalama wao na kwamba watapewa hadhi rasmi ya ukimbizi. Hata hivyo, kuna wasiwasi wa kibinadamu kwani Burundi tayari inahifadhi wakimbizi wapatao 90,000, wengi wao wakitoka DRC kutokana na mizozo ya awali.
Mvutano wa kikanda na udhamini wa Rwanda
Vita hivi vimeongeza mvutano wa kidiplomasia, ambapo DRC inaituhumu Rwanda kwa kuchochea mgogoro kwa kuunga mkono waasi wa M23. Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner, alizitaka klabu za Arsenal, Bayern Munich, na Paris Saint-Germain (PSG) kusitisha mikataba yao ya udhamini na "Visit Rwanda," akiziita "zilizojaa damu." Rwanda ilikanusha tuhuma hizo, ikiziita jaribio la kupotosha ukweli na kudhoofisha ushirikiano wake wa kimataifa.
Umoja wa Mataifa umearifu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na mauaji ya haraka, ukatili wa kingono, na mashambulizi dhidi ya kambi za wakimbizi.
Soma pia: Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu vita vya kikanda katika mkutano wa AU
Rwanda, kwa upande wake, inadai inajilinda dhidi ya jeshi la DRC ambalo linashirikiana na wanamgambo wa Kihutu, baadhi yao wakiwa wahusika wa mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda na baadaye wakakimbilia DRC.
Waasi wa M23, wanaosemekana kuungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 wa Rwanda, wameapa kuendelea kusonga mbele, wakitishia hata kufika Kinshasa, zaidi ya kilomita 1,600 kutoka mashariki mwa DRC.
Mafanikio yao ya haraka katika wiki za hivi karibuni yamefufua kumbukumbu za Vita ya Pili ya Kongo (1998-2003), vita vilivyojihusisha na mataifa mengi ya Afrika na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu.
Mustakabali wa mashaka kwa wakimbizi na kanda
Huku maelfu ya wakimbizi wakiendelea kumiminika Burundi kila siku na mgogoro ukiendelea kushamiri, kanda hii inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu. Juhudi za kimataifa za kusaka amani bado zinakwama, huku wasiwasi ukiongezeka juu ya uwezekano wa vita vikubwa zaidi.
Soma pia: Bayern Munich yakosolewa dili lake la Visit Rwanda
Kwa sasa, Burundi inajikuta katikati ya mgogoro huu, ikihangaika kuhifadhi idadi inayoongezeka ya wakimbizi huku ikinavigate hali tete ya kisiasa katika eneo la Maziwa Makuu.
Chanzo: AFP, RTRE, DPA