1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya maambukizi ya virusi vya corona vyapungua China

Daniel Gakuba
12 Februari 2020

Maafisa wa China wamesema idadi ya visa vipya vya maambukizi ya homa ya virusi vya corona imeshuka tena leo, ikiashiria, ingawa kwa tahadhari, kuwa mripuko wa ugonjwa huo hatari huenda ukamalizika mnamo miezi ijayo.

https://p.dw.com/p/3XeVZ
China Coronavirus l Zhong Nanshan - Wissenschaftler
Picha: Reuters/China Daily

 

China imesema idadi ya visa vipya vya maambukizi ya homa ya virusi vya corona vilivyosajiliwa leo Jumatano ni ya chini zaidi tangu mwezi Januari. Hali hiyo inaupa uzito utabiri wa maafisa wakuu wa afya nchini humo, kwamba mripuko wa ugonjwa huo waweza kuwa umemalizika ifikapo mwezi Aprili. Wataalamu wa kimataifa hata hivyo, wameonya kwamba bado ni mapema kuwa na matumaini ya namna hiyo.

Taarifa iliyotolewa na mshauri mkuu wa masuala ya afya nchini China Zhong Nanshan, imeeleza kuwa ripoti zinaonyesha kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya corona katika mikoa mbali mbali ya nchi hiyo, na kwamba dalili zinaashiria kuwa baada ya mwezi huu wa Februari kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo itapungua.

China Coronavirus l Zhong Nanshan - Wissenschaftler (Getty Images/AFP/Str)
Zhong Nanshan, mtaalamu wa magonjwa yatokanayo na virusiPicha: Getty Images/AFP

Matumaini yenye tahadhari

Masoko ya fedha na mitaji ulimwenguni yamepokea vyema taarifa hiyo, licha ya tahadhari kutoka kwa wataalamu wa kimataifa waliotishwa na namna homa hiyo ilivyoenea kwa kasi na kuuwa watu zaidi ya 1,100, wote, isipokuwa wawili tu, wakiwa wakaazi wa China Bara.

Zhong ambaye utabiri wake wa siku zilizopita haukuwa sahihi, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa anaamini ifikapo mwezi Aprili mwaka huu, mripuko wa homa hii hatari utakuwa umemalizika, ingawa kuanza tena kwa shughuli za usafiri kunawapa wasiwasi baadhi ya watu.

''Kwa wakati huu, watu wengi wanaanza safari kurejea sehemu zao za kazi, na hili linasababisha wasiwasi juu ya uwezekano wa kuzidisha kitisho cha maambukizi mapya. Lakini kwa kuzingatia hali ya sasa, siamini kwamba hofu yao ina msingi.'' Amesema Zhong.

Mashaka mitandaoni

Japan Yokohama Kreuzfahrtschiff Princess Diamond mit Corona-Kranken
Meli ya Diamond Princess iliyowekwa karantini baada ya wasafiri wake kukutwa na homa ya virusi vya corona.Picha: picture-alliance/Xinhua/Du Xiaoyi

Tangazo la matumaini la viongozi halijazuia mashaka miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China juu ya uaminifu wa takwimu zinazotolewa, baada ya hatua ya serikali kubadili maelekezo katika mfumo wa kukusanya data za maambukizi ya homa ya virusi vya corona.

Wakati huo huo, idadi ya wasafiri walioambukizwa virusi vya corona katika meli ya anasa ya Diamond Princess imepanda na kufika watu 175, kufuatia kugunduliwa kwa visa vipya 39. Meli hiyo iliwekwa chini ya karantini nje ya bandari ya Yokohama, Japan tarehe 3 Februari. Afisa mmoja wa kufuatilia karantini hiyo ni miongoni mwa wagonjwa wapya.

rtre, ape