Vipi taasisi za Kikristo na Kiislamu husaidia jamii
30 Mei 2008Mpende jirani yako kama unavyojipenda - na tenda wema kwa jamii - ni nguzo isiyokutikana katika dini ya kikristo peke yake.Kwani hata dini zingine kama vile ya Kiislamu, waumini wake wanahimizwa kushughulikia wanyonge, masikini na jamii nzima.
Kwa maoni ya Askofu Franz Vorrath kutoka mji wa Ujerumani Essen,hali ya wasi wasi na hofu iliyopo kati ya Wakristo na Waislamu ni hali inayokutikana hata katika huduma za kijamii katika dini zote mbili.Anasema,kwa upande mmoja,Waislamu wanaamini kuwa taasisi za makanisa kama vile chekechea,shule na hospitali ni vyombo vinavyotumiwa kueneza Ukristo;upande mwingine,Wakristo wengi wanaamini kuwa dini ya Kiislamu haijihusishi na masuala ya kijamii.Na mkutanoni imedhihirika kuwa hoja zote mbili hazina msingi.
Askofu Franz Vorrath anaesimamia pia Halmashauri ya mkutano wa maaskofu wa Ujerumani inayohusika na midahalo kati ya dini mbali mbali,kwanza amekumbusha mzizi wa amri ya Mungu kumpenda jirani na vipi Caritas-taasisi ya kanisa ilivyoanzishwa.Akamnukuu Mathias katika Injili: "Mlichowatendea ndugu zangu mmenitendea na miye pia.Kumhudumia jirani yako ni amri ya Mungu,bila ya kujali ikiwa anaamini Mungu au la."
Taasisi ya kanisa,Caritas inayotoa misaada,ilizinduliwa wakati wa shida katika karne ya 19 nchini Ujerumani. Wakristo walihimizwa kujijumuisha na kuwasaidia masikini na wagonjwa.
Na hata katika Quran kuna hadithi nyingi zinazoshauri kumshughulikia jirani yako.Profesa Abdullah Takim wa Fani ya dini ya Kiislamu kwenye chuo kikuu cha Frankfurt alinukuu aya ya Quran inayosema,"Huwezi kuwa muumini kabla ya kwanza kumshughulikia na kumuenzi jirani yako."
Nadeem Elias wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani anaeleza kuwa hata katika dini ya Kiislamu kuna mashirika ya kuhudumia jamii kama Caritas inavyofanya. Akayataja mashirika ya misaada ya misikiti inayokusanya fedha kuwasaidia watu wenye shida.Misikiti yote 2,000 nchini Ujerumani ina mashirika kama hayo.
Mafunzo ya Kiislamu yanashadidia anaetaka kuimarisha uhusiano katika jamii yake anaimarisha uhusiano wa jamii kwa jumla.