Viongozi washtumiwa kusababisha wakimbizi kukimbia nchi zao
18 Julai 2019Balozi wa Ujerumani nchini Uganda amewashtumu viongozi wa nchi wanaosababisha raia wao kukimbilia nchi nyingine na kuwa wakimbizi. Balozi huyo amesema mtu kuwa mkimbizi si jambo la kimaumbile na wakimbizi wapatao milioni 70 duniani wanaweza kurudi makwao ikiwa viongozi watajenga na kuhakikisha mazingira ya amani na usalama katika nchi zao.
Serikali ya Ujerumani kupitia balozi wake nchini Uganda Dr. Albecht Conze, imesisitiza kwamba kuna uwezekano wa mataifa yote duniania kuepusha hali ya watu kuzimbikia nchi zao kutokana na vita na ukosefu wa amani na usalama ambayo vyanzo vyake ni viongozi wa kisiasa wanaozingatia tu kulinda maslahi yao badala ya maisha ya raia wao.
Balozi huyo aliyasema katika uzinduzi wa mpango wa kuwezesha wakimbizi na wenyeji wao kaskazini magharibi mwa Uganda kuendesha shughuli za kipato na hivyo kujitegemea.
Hii ni baada ya serikali ya Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya kusitisha kwa muda utoaji misaada kwa mipango ya kuwahudumia wakimbizi wakipinga mienendo ya ufisadi miongoni mwa mashirika yanayoshughulikia wakimbizi pamoja na serikali ya Uganda.
Amefafanua kuwa wamerejelea kutoa misaada hiyo chini ya mpango ujukilanao kama RISE lakini wakifuata mkakati wa kushirikiana moja kwa moja na serikali za mitaa katika wilaya tatu pamoja na makundi ya wakimbizi na wenyeji badala ya kupitia kwa serikali kuu.Mpango huo utagharimu euro milioni 20.
Waziri wa serikali za mitaa Uganda Jennifer Namuyangu amepongeza hatua ya serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa jumla kurejelea kutoa misaada akiahidi kwamba wanaendelea kurekebisha mifumo ya kuwashughulikia wakimbizi ili kuepusha vitendo vya ufisadi.
Kwa sasa eneo la Kaskazini Magharibi mwa Uganda lina wakimbizi zaidi ya laki saba wengi wao wakitokea Sudan Kusini. Licha ya viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kusaini mkataba wa amani bado kuna hali ya sintofahamu na kila kukicha kuna raia wa nchi hiyo wanaokimbilia Uganda. Kwa ajili hii ndipo watoaji misaada wanasema hawawezi kufumbia jicho madhila ya wakimbizi ila wawasaidie kujiendeleza kimaisha ugenini sambamba na kusaidia jamii za wenyeji kuishi kwa amani nao.