1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wakaribia kuafikiana juu ya uongozi

Daniel Gakuba
2 Julai 2019

Duru kutoka Brussels zinasema kuwa Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk atampendekeza waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen katika wadhifa wa rais wa Halmashaur ya Ulaya, katika juhudi za kuumaliza mkwamo.

https://p.dw.com/p/3LTTa
Eurofighterabsturz Ursula von der Leyen
Picha: picture-alliance/dpa/J. Büttner

Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Ujerumani, DPA, vyanzo vya kuaminika vimethibitisha kuwa Bi Ursula von der Leyen anaungwa mkono na Ufaransa na Uhispania, na ni sehemu ya mpango unaomweka waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel katika nafasi ya kurithi urais wa Baraza la Ulaya baada ya Donald Tusk kumaliza muda wake, na pia waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Josep Borrell akitarajiwa kupokea mikoba ya mkuu wa sasa wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini.

Ursula von der Leyen ni waziri wa sasa wa ulinzi wa Ujerumani, akitoka chama cha Christian Democratic Union cha Kansela Angela Merkel. Akizungumzia hatua hiyo ya hivi karibuni, Kansela Angela Merkel amesema hivi sasa ni muda wa kutazama mbele.

"Kila  mmoja anapaswa kusogea mbele.Na katika hilo ninamaanisha kila mmoja.Pana uwezekano wa kufikia suluhisho na tunao wajibu wa kutafuta  suluhisho na katika moyo huo nafanya juhudi kwa uthabiti".

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekuwa wakipambana kwa mara nyingine leo kumaliza mkwamo wa kuaibisha, kwa kukubaliana juu ya mgombea kwenye nafasi muhimu ya urais wa Halmashauri inayochukua maamuzi ya umoja huo, pamoja na wa baraza linaloratibu vikao vya viongozi hao.

Europawahl l Polen - Donald Tusk, Präsident des Europäischen Rates, gibt seine Stimme ab
Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk Picha: Reuters/K. Pempel

Kikao cha leo kilicheleweshwa kwa masaa manne, wakati rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk akifanya mazungumzo katika makundi madogodogo, kutafuta maridhiano baina ya nchi na makundi yanayowania nafasi hizo zenye ushawishi. Soma zaidi...

Umoja wa Ulaya unajaribu uwezavyo kujionyesha kuwa bado ni jumuiya yenye umoja, baada ya kambi mbili za vyama vilivyoshika hatamu za uongozi wake kwa miongo mingi kupoteza wingi wake katika uchaguzi wa bunge la Ulaya wa mwezi Mei.

Changamoto kubwa imekuwa kuyapata majina ya wagombea wa nchi 28 wanachama, ambayo yanawakilisha uzani wa kimajimbo, wa kijinsia na pia unaoweka usawa baina ya nchi kubwa kwa idadi ya watu, na zile zilizo na watu wachache.

Mapema leo ilionekana kama waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi Frans Timmermans alikuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo muhimu ya uongozi wa halmashauri ya Ulaya, lakini nchi za Mashariki mwa Ulaya, zikiwemo Jamhuri ya Chech, Slovania, Hungary na Poland zilikataa katakata kumuunga mkono.

Vyanzo: dpae,afpe